25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

URAIS WA AFRIKA KUSINI UNAPOTIBUA UTULIVU WA KISIASA

NA RAS INNO,

KILICHOTOKEA Alhamisi iliyopita katika Bunge la Afrika Kusini ambacho kilisababishwa na wanasiasa wahafidhina wa mrengo wa kushoto wa upande wa upinzani waliovuruga hotuba ya ya Rais Jacob Gedleyihlekisa Zuma, maarufu kama ‘JZ’ ni kikonyo tu cha figisu kubwa ya kisiasa inayoendelea katika taifa hilo hususanI katika kuelekea kumalizika muda wa utawala wake uliogubikwa tuhuma za ufisadi anazoelekezewa kwa matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma.

Sakata zima lilihanikizwa na wabunge wanachama wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), waliomtupia makombora ya shutuma Rais huyo na kusababisha kukatiza hotuba yake mara kwa mara. Inavyoelekea Zuma aliitarajia hali hiyo kwa kuwa aliidhinisha zaidi ya askari 400 kujumuika katika vikosi vya ulinzi nje ya jengo la Bunge na kushutumiwa na wapinzani kuwa analigubika Bunge hofu ya kijeshi.

Spika wa Bunge, Baleka Mbete, alilazimika kuamrisha wabunge wa EFF watoke nje baada ya kiongozi wao mwingi wa makeke, Julius Malema, kudai kwamba Zuma ameoza kisiasa hoja iliyoungwa mkono na kiongozi wa chama kingine cha upinzani Democratic Alliance (DA), Mmusi Maimane, aliyesema kuwa Zuma hafai kuendelea kutawala kutokana na kuchafuka kwa tuhuma za ufisadi.

Katika siku za hivi karibuni hotuba za Zuma bungeni zimezua hamkani kubwa lakini Alhamisi iliyopita ilikuwa kubwa zaidi kwa ngumi kufumuka na kugeuza chombo hicho cha kutunga sheria kuwa ulingo wa masumbwi. Nje ya Bunge katika mitaa ya jirani polisi walifyatua mabomu ya vitisho ili kuwatawanya wafuasi wa EFF na ANC waliotaka kukabiliana, baina ya pande mbili zinazompinga na kumuunga mkono Rais.

Chama tawala cha ANC kinahodhi asilimia 60 ya idadi ya wabunge wote wa Bunge hilo lenye wabunge 400, lakini hiyo haimpi mazingira mazuri Rais Zuma ambaye anapingwa hata ndani ya chama chake kutokana na staili yake ya kufanya uzengezi kwa kuvutia kamba katika mambo yanayomlinda yenye maslahi binafsi kwake. Katika hotuba yake Rais Zuma alizungumzia nguvu ya uchumi na tija miongoni mwa wananchi wote, ambayo bado kwa sehemu kubwa inahodhiwa na ‘Weupe’ miongo miwili baada ya kumalizika kwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, kwamba uhuru wa kisiasa bila uhuru wa kiuchumi hauna maana.

“Leo tunaanza ukurasa mpya wa mabadiliko muhimu ya kiuchumi, tukidhamiria kutenda zaidi kuliko kuongea kwa mchakato wa kivitendo” Kauli ambayo inaashiria mambo kadhaa hasi yanayoikosesha nguvu: kwanza inakuja katika wakati ambao anakaribia kumaliza muda wake madarakani hivyo dhamira anayoitamka inawezekana kuwa kama ishara tu na si mkakati kamili.

Lakini jambo la pili ni kuchafuka kwa hadhi yake kutokana na tuhuma za ufisadi hususani kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kunadhifisha hekalu lake katika kitongoji cha Nklanda, jambo la tatu ni uzengezi wa kificho anaojaribu kuufanya ili kuhakikisha mmojawapo kati ya waliowahi kuwa wake zake, Nkosazana Dlamini, anateuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao akitarajia fadhila za ‘mapenzi ya kale’ katika kufunikiwa maovu yake kwa dhana kuwa mtalaka siku zote haombwi upya mahusiano, bila kusahau vigogo wengine pia wanaitaka nafasi hiyo akiwamo Makamu wa Rais Cyril Ramaphosa.

Figisu hizo zinasababisha mvutano ndani ya chama hicho kinachozidi kupasuka katika makundi mawili kati ya wanaomuunga mkono na wanaompinga Rais Zuma, hivyo kukipunguzia nafasi ya ushindi wa kishindo uliozoeleka tangu Nelson Mandela alipokuwa Rais wa kwanza mweusi wa Taifa hilo.

Kwa mujibu wa Katiba ya Taifa hilo Rais ambaye ni mkuu wa nchi na Serikali huchaguliwa na Bunge kutokana na jina pendekezwa kutoka katika chama kilichopata wingi wa viti kwenye uchaguzi, ambaye anaweza kuhudumu si zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano (miaka 10) na anapochaguliwa lazima awe mbunge wakati jina lake linapendekezwa. Kimsingi Afrika Kusini huchagua nafasi za uongozi ambazo baadaye chama husika kilichokubaliwa zaidi hutaja wanaowataka wakalie viti hivyo, nafasi inayoachwa wazi huzibwa na chama hicho hicho ambapo chama kina mamlaka ya kumrudisha kutoka kuhudumu nafasi mwanachama wake wanayehisi hatimizi majukumu kadiri inavyopaswa au kutokana na sababu nyingine hususani za kimahakama.

Hiyo ilimtokea Rais Thabo Mbeki aliyelazimika kutangaza kujiuzulu Septemba 20, 2008, baada ya kuondolewa na Kamati Kuu ya ANC kutokana na uamuzi wa mahakama iliyomtia hatiani kwa kuingilia mamlaka ya mhimili huo kwa tuhuma alizomzushia Jacob Zuma ambazo zilitupiliwa mbali kwa rufaa ya mahakama kuu.

Baada ya Mbeki kulazimika kujiuzulu aliyekuwa Waziri wa mawasiliano, Ivy Matsepe-Casaburri, aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo kwa muda wa saa 14 wakati mchakato wa kumtafuta Rais mwingine ukitimizwa akachaguliwa Kgalema Motlante, kabla ya Jacob Zuma kuingia madarakani Mei 9, 2009, atakayemaliza muhula wake wa pili wa ukomo mwaka 2019 uchaguzi mkuu utakapofanyika. Kati ya maraisi wote waliohudumu kwenye nchi hiyo marais wastaafu walio hai ni wawili tu, Mbekhi na Motlante, Matsepe-Casaburri alifariki mwaka 2009 na Nelson Mandela alifariki mwaka 2013.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles