28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

HII VITA HII YA DAWA ZA KULEVYA…

NA LEAH MWAINYEKULE,

NI jambo lisilokwepewa kulijadili wiki hii.  Vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo imeanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, imekuwa gumzo kila kona.  Licha ya yeye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pekee, vita aliyoamua kukabiliana nayo imeibua tafrani pembe zote za nchi na pengine hadi nje ya nchi.

Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Makonda kwa uthubutu wake na ujasiri wake wa kuamua kulivalia njuga suala la matumizi ya dawa za kulevya.  Anastahili pongezi, kwani ni vita ambayo imeshawashinda wengi, lakini yeye akiwa ni Mkuu wa Mkoa tu, ameamua kuivaa ‘head-on’.

Mengi yamezungumzwa tangu siku Makonda alipoamua kuita baadhi ya watu kwenda kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano.  Mengi yalisemwa kutokana na ‘staili’ ya Makonda kuita ‘watuhumiwa’ kupitia vyombo vya habari, badala ya njia ya kisheria ambayo imezoeleka kwa watuhumiwa kuitwa na polisi wenyewe.

Wapo waliomsema vibaya, wapo waliompongeza.  Binafsi, sina uhakika kama alilolifanya ni jema ama baya, isipokuwa tu ninayo maswali mengi sana kuhusiana na hatua yake ya kutaja watu hadharani na pia kuhusu kauli za mashambulizi zinazoelekezwa kwake.

Baadhi ya wasanii wetu wa hapa nchini walikuwa wa kwanza kabisa kutajwa majina yao hadharani na kuitwa polisi.  Hilo lilipotokea, wapo waliosema vibaya, wapo pia waliofurahia.

Baadaye, majina yakatolewa mengine ya watu wenye hadhi hapa nchini, wakiwamo wamiliki wa hoteli kubwa, wafanyabiashara maarufu, mchungaji mmoja na hata baadhi ya wabunge.  Hapo, ghafla mashambulizi dhidi ya Makonda yakazidi kuongezeka kutoka kwa watu ambao wakati wasanii wakitajwa, wao walikuwa wamenyamaza kimya; lakini walipotajwa watu wa kiwango kingine, wao wakaibuka.

Imefikia hatua, Makonda amekuwa hata ‘topic’ ya kujadiliwa bungeni, huku waheshimiwa hao wakitaka kijana huyo aitwe kujieleza.  Bado sijaelewa aitwe kwa sababu ipi, lakini ninachokijua ni kwamba yeye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kuitwa Dodoma kwa ajili ya kujieleza ni kama waheshimiwa hao kulazimisha jambo ambalo sidhani ni la kwao.

Sitaki kumtetea Makonda kutokana na hatua yake ya kujigeuza kuwa polisi na kutaja majina ya watu hadharani akiamuru wafike polisi kwa maelezo.  Sina hakika kama hiyo ni kazi yake, hata chini ya kofia ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa. 

Lakini pamoja na kutotaka kumtetea kwa hilo, bado najiuliza kwamba, kwanini alilifanya?  Kwanini alitaja majina ya watu hadharani wakati yeye si polisi na bila kufuata taratibu za kisheria?  Kwanini aliamua ‘kuwachafua’ na kusababisha watu kuwaona waliotajwa wote kama watumiaji wa dawa hizo za kulevya? Je, huo ni mkakati maalumu anaoufanya kwa ajili ya kuwapata ‘mapapa’ wenyewe wa dawa za kulevya?  Au kwa kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya ni ngumu, basi huenda ameona hiyo ndiyo njia mwafaka zaidi ya kukabiliana nayo?  Bado najiuliza.

Neno moja kwa waheshimiwa wabunge: Ni kweli kwamba utaratibu wa kuita tu watu kupitia vyombo vya habari na kuwatuhumu kuhusika na dawa za kulevya, haupendezi.  Ni kweli vile vile kwamba mtu akitajwa hadharani, hata kama hahusiki, watu waliomzunguka wataamini kwamba anahusika (anakuwa tayari na madoa, amechafuliwa). 

Lakini vile vile, ni kweli kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya ni ngumu na unapoanza kumsema vibaya mtu aliyejitoa kuikabili, kwa kudai kwamba hata yeye mwenyewe anatakiwa kuchunguzwa kutokana na kuwa na mali za ghafla zisizoelezeka, hiyo si haki.  Inatufanya sisi wengine tujiulize, kwanini unatokwa povu jingi na kuibua mambo ambayo hayana uhusiano?  Ulikuwa wapi siku zote kuzungumzia “utajiri” wake?  Kwanini sasa?

Vile vile, waheshimiwa wanapokuwa wanatumia nguvu nyingi kumjadili Mkuu wa Mkoa mmoja tu anayepambana na uharamia ulioko mkoani kwake, hilo nalo linaibua maswali.  Walipotajwa wasanii, mlikuwa wapi?  Ninyi ni wawakilishi wa wananchi wote – wakiwamo wasanii pia  au mnajiwakilisha wenyewe?

Vita hii ni ngumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles