25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

LIPUMBA: MAALIM SEIF NJOO TUZUNGUMZE

Na ASHA BANI

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba amemwomba Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuondoa kesi mahakamani ili wafanye mazungumzo ya maridhiano.

Profesa Lipumba, aliyasema hayo jana katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na Televisheni ya AZAM na kuongozwa na mtangazaji mkongwe, Tido Mhando,aliyetaka kufahamu  suluhisho la mgogoro wao ndani ya chama hicho ni lipi.

Akijibu swali hilo, Profesa Lipumba alisema suluhisho la mgogoro huo ni wao kufanya mazungumzo, kwa sababu ni wanasiasa wakongwe na wametoka mbali.

Alisema  kama waliweza kusulushisha na kupata mwafaka wa mgogoro mzito kati ya CUF na CCM na huu wa sasa ndani ya chama chao unawezekana bila kutumia mahakama.

“Ni sisi kuzungumza, maalim  Seif ni mkongwe alizungumza mgogoro wa Zanzibar kutafuta mwafaka kwa kumshirikisha Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula, iweje mimi mwenyekiti wake ambaye tupo pamoja muda mrefu tusifanye mazungumzo tufikie mwafaka?,’’alihoji Profesa Lipumba.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema yeye ni mwenyekiti halali ndani ya chama hicho, alichaguliwa na mkutano halali na Katibu Mkuu wake ni Maalim Seif tangu mwaka 2014.

Mtangazaji pia alimwuliza yeye ni mmoja wa waanzilishi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)), lakini ameishia kwenye Katiba ni kwa nini?

Akijubu swali hilo, Profesa Lipumba alisema umoja huo ulikuwa na lengo la kutetea rasimu ya Katiba ya wananchi, lakini baadaye wakasema wafanye majadiliano mengine ya kisiasa.

Profesa Lipumba alisema katika muungano huo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilivizidi kete vyama wanachama wa umoja huo kwa kutumia utaratibu wa kuwaondoa kisiasa washirika wenzao.

Alisema katika mikutano mbalimbali ya hadhara, Chadema walikuwa wakiwaambia wananchi kwamba kitasimamisha wagombea wake kupitia Ukawa, pasipokutaja vyama vingine.

‘’Ukawa tulikuwa vyama vinne,wenzetu wa chadema katika ushirikiano huu wao wafunike vyama vyote wabakie wao tu hasa  kwa upande wa Tanzania Bara katika mashirikiano ya uchaguzi,’’ alisema Profesa Lipumba.

Alisema jambo lililomkera zaidi, ni ushirikiano wao  na Ukawa ambao alidai Maalim Seif  alikuwa akifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa siri, huku yeye akipewa taarifa za mazungumzo baadaye.

Alipoulizwa kama haoni kulikuwa na nia njema kwa sababu Chadema nguvu zake ziko Bara na CUF ziko Zanzibar na kama wangechukua dola wangekuwa wamoja.

Akijibu swali hilo, Profesa Lipumba alisema. “Kama   Chadema walikuwa na mkakati huo, jambo zuri wangeliweka mezani na kulipa nguvu ndani ya chama kujua mkakati huo unakwendaje.

Profesa Lipumba alisema alikereka zaidi kwani, masuala mbalimbali yalikuwa ukifanyiwa uamuzi na katibu mkuu bila yeye kushirikishwa.

“Tulitarajia baada ya nyinyi kumaliza mchakato wa Katiba mngeungana na kuwa chama kimoja chenye usajili, ili kuiondoa CCM,” alihoji Tido.

Akijibu swali hilo, Profesa Lipumba alisema. “Waliojitoa kuingia upinzani walifanya kazi kubwa na kazi ngumu, japo kulikuwa na tatizo la kisheria kufanya muungano wa chama kuwa kimoja,” alisema.

Alisema kinachohitajika, ni kuwa na mkakati wa awali kuwa na nguvu moja ya kuimarisha chama kwa malengo ya siasa kufanana kwa mfumo na haki sawa kwa wote.

Kuhusu kuteuliwa kuwa mgombea urais wa umoja huo, alisema yeye alikuwa anajiamini hivyo kama kiongozi kutokana na uzoefu wake alionao hasa katika kutatua matatizo yanayowakabili wananchi.

Alisema hata kama asingegombea yeye, walikubaliana ndani ya umoja huo, kuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa angeweza kupeperusha vyema bendera ya Ukawa.

“Tulikubaliana Dk.Slaa awe mgombea wetu lakini mambo yalibadilika katika mazingira tata,”alisema.

Alisema baada ya kupanga kukutana na wabunge na viongozi wengine ili waweze kumpitisha Dk. Slaa, lakini Mbowe alikuwa akimwandama na kumtuhumu kwmaba yeye anataka nafasi hiyo.

‘’Tulikutana na Mbowe na wabunge wakati hatujafikia uamuzi wa kumpa Dk. Slaa kugombea nafasi ya urais kupitia Ukawa…Mbowe alinishambulia mara kadhaa kuwa sisi tunalengo la kuchukua mabaki CCM,”

KUMPOKEA LOWASSA

Alipoulizwa nani alikuwa mstari wa mbele kumpokea Edward Lowassa kutoka CCM, Profesa Lipumba alisema viongozi wote walihusika na mchakato wa kumshawishi ajiunge na Ukawa, lakini si kwa lengo la kugombea urais.

“Tulimkaribisha Lowassa, alisema anakuja na watu wengi wa kujiunga na Ukawa, hatukusema anakuja kuwa mgombea urais wetu…tulimkaribisha kuleta mabadiliko katika nchi si urais.

“Tulimkaribisha kupata watu wengi,waliaanza kumleta Lowasa ni Chadema wakati tulishakubaliana nyumbani kwangu kwamba Dk. Slaa agombee,” alisema Profesa Lipumba.

UCHAGUZI

Alipoulizwa kuwa aliuonaje mtikisiko katika wagombea wa uchaguzi 2015 , alisema aliona ni wagombea wawili  waliokuwa na mganga wao mmoja TB Joshua.

Alikiri, licha ya kuwa wagombea wawili mganga mmoja palikuwa na mvuto na ushindani ulikuwa wagombea hao kutoka chama kimoja cha CCM.

KUJIUZULU KWAKE

Alisema hakuwa na nia ya kurudi katika chama hicho, bali wajumbe kutoka Bara na Zanzibar walimfuata kumtaka arudi kwa sababu kilikuwa kimebaki chama cha kutoa matamko mapesi.

Alisema alifuata utaratibu wa kurudi, ikiwa ni pamoja na kuandika barua ya kuomba kurudi.

Alipoulizwa kama hakuona haikuwa sawa kujifuta kazi miezi kumi, kisha kuomba kurudi tena, alijibu kwa kusema Katiba ya CUF, ibara ya 117 iko wazi inasema amechaguliwa  na mkutano mkuu, ameandika barua  kwa mkutano mkuu hakujibiwa lolote hivyo alikuwa na haki ya kurudi tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles