26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

SERIKALI YATAJA MAENEO 55 YENYE UPUNGUFU WA CHAKULA

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

SERIKALI imesema halmashari zenye upungufu wa chakula nchini, zimeongezeka kutoka 43 hadi halmashauri 55.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni jana na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, alipokuwa akiwasilisha bungeni kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula na lishe nchini kwa mwaka 2016/2017.

“Katika Bunge la 10, Serikali ilitoa kauli na kusema upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/17, kitaifa uzalishaji wa chakula utafikia tani 16,172,841 wakati mahitaji ya chakula kwa mwaka huo ni tani 13,159,326 na hivyo nchi kuwa na ziada ya tani 3,013,515.

“Kati ya tani hizo za ziada, tani 1,101,341 ni mazao ya nafaka na tani 1,912,174 ni mazao yasiyo ya nafaka. “Kwa maana hiyo, nchi ilikuwa na utoshelevu wa chakula kwa asilimia 123.

“Pamoja na hali nzuri ya chakula kitaifa, kulikuwa na halmashauri 43 ambazo zilikuwa na maeneo yenye upungufu wa chakula.

“Mwezi Januari mwaka huu, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya uhakika wa chakula na lishe, imekamilisha tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe nchini kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

“Pia walikuwamo wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Wizara ya Afya kupitia taasisi yake ya Chakula na Lishe (TFNC).

“Tathmini hiyo, ilibainisha kuwa, kuna halmashuri 55 zenye upungufu wa chakula nchini na jumla ya tani 35,491 za chakula zinahitajika ili kukabiliana na upungufu wa chakula kati ya mwezi Februari na April mwaka huu,” alisema.

Hata hivyo Dk. Tizeba hakuzitaja halmashauri hizo zenye upungufu wa chakula zaidi ya kueleza kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo.

Pamoja na hayo, alisema watu 118,603 wasio na uwezo wa kupata chakula, watahitaji tani 3,549 za chakula kwa bei nafuu haraka.

Ili kukabiliana na athari za ukame ulioyakumba baadhi ya maeneo nchini, Dk. Tizeba alisema Serikali itaendelea kuchukua hatua ili kuhakikisha hali ya chakula inazidi kuimarika.

Alizitaja hatua hizo, kuwa ni pamoja na kusimamia usambazaji wa mbegu zinazostahamili ukame, kuhamasisha wakulima kulima mazao ya aina ya mizizi, mtama na uwele, kuendelea kuhifadhi kwa uangalifu chakula kilichopo na kuhamasisha taasisi binafsi kununua mazao ya chakula katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika maeneo yenye uhaba.

“Pia, tunahimiza usindikaji wa mazao ya chakula kwa kuyaongeza thamani, kuwashauri wananchi kutumia kwa uangalifu chakula kilichopo na wakuu wa mikoa na wilaya wawahimize wananchi watumie mbegu zinazokomaa mapema.

“Pamoja na kuyasema hayo, napenda kusisitiza kwamba, Serikali itaendelea kufuatilia hali ya chakula na lishe nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha hali ya chakula na lishe nchini inaridhisha zaidi,” alisema Dk. Tizeba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles