33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lamkingia kifua Zitto

Zitto_Kabwe_2011Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu
OFISI ya Bunge imesema haijapata barua yoyote kuhusu kuvuliwa uanachama kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Kauli ya hiyo ya Bunge imekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza kumvua uanachama Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema kutokana na hali hiyo, Zitto bado ni mbunge halali wa Kigoma Kaskazini na kwamba anapaswa kuendelea na shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
“Zitto ni mbunge wa Kigoma Kaskazini, kwa sababu mpaka sasa hatujapewa barua yoyote ya kuonyesha kuwa amefukuzwa uanachama na chama chake, kwa hiyo ofisi ya Bunge inamtaka kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema Dk. Kashilillah.
Alisema ikiwa Chadema imeamua kumvua uanachama, wanapaswa kufuata utaratibu wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kumwandikia barua Spika wa Bunge kumjulisha uamuzi wao ili aweze kuchukua hatua nyingine za kisheria.
Dk. Kashilillah alisema miongoni mwa hatua ambazo Spika atachukua, ni pamoja na kumwandikia barua msajili wa vyama ili aweze kufanya uchunguzi na kupitia upya kanuni ya chama hicho kuangalia kama walifuata utaratibu wa kisheria wa kumvua uanachama.
“Baada ya hapo, msajili anamwandikia barua Spika kumjulisha hatua zote za kisheria zilizotumiwa na chama wakati wa kufanya uamuzi huo ili aweze kuipitia.
“Akimaliza, Spika anawaandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwataarifu suala hilo,” alisema Dk. Kashililah.
Katibu huyo wa Bunge alisema ikiwa itabainika chama hakijafuata utaratibu wa kumvua uanachama, sheria inampa nguvu Spika wa Bunge kubatilisha au kutengua uamuzi wa kumvua ubunge.
Alisema suala la kuvuliwa ubunge kwa Zitto liko mikononi mwa Spika pale atakapokuwa amekabidhiwa barua rasmi ya kumjulisha uamuzi wa chama.
Dk. Kashilillah alisema tukio kama la Zitto liliwahi kutokea kwa mmoja wa wabunge katika Bunge la sasa la 10, ambapo Spika Anne Makinda aliangalia kanuni zilizotumika za kumvua uanachama mbunge huyo na kuona hazijafuata utaratibu kwa mujibu wa sheria.
Alisema kutokana na hali hiyo, Spika alitengua uamuzi wa chama na kumwacha hadi sasa kuendelea na majukumu yake ya kibunge.
“Tukio kama la Zitto liliwahi kutokea katika kipindi hiki hiki cha Spika Makinda, lakini aliweza kutengua uamuzi wa chama wa kumvua ubunge na mpaka sasa bado anaendelea na majukumu yake kama kawaida,” alisema.

ZITTO AZUNGUMZA
Kwa upande wake, Zitto alisema anaendelea na kazi kama kawaida hadi Chadema watakapofuata taratibu za kisheria za kumvua uanachama.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, alisema wakati uamuzi huo unafanyika hakuwa na habari ya kuendelea kwa kesi hiyo jambo ambalo lilimfanya aendelee na shughuli za Kamati ya Bunge kama kawaida.
“Ninaendelea na kazi kama mnavyoniona na hadi sasa sijapewa barua yoyote ya kunitaarifu kuwa mimi si mwanachama, nasikia tu kupitia taarifa mbalimbali kuwa uamuzi huo umefikiwa jana (juzi).
“Uamuzi wowote unaotolewa na chama una taratibu zake, hivyo basi suala hilo lazima Spika ajulishwe kwa kuandikiwa barua na yeye akiridhika ataniandikia barua,” alisema Zitto.
Alisema kazi yake ni kuwatumikia wananchi na siyo kukaa na kujibizana na chama kwa kuwa hakulelewa hivyo kisiasa.
“Mimi siwezi kujibizana na chama kwani sijalelewa hivyo, sina muda wa kufanya siasa za namna hiyo, ninachoweza kuwaambia ni kwamba huwezi kunifananisha mimi na mbunge mwingine yeyote kwa uchapakazi, kwa sababu majukumu yangu mnayaona.
“Muhimu kwangu mimi ni kufuatilia masuala ya umma tofauti na wengine ambao kazi yao ni kufuatilia na masuala ya watu binafsi,” alisema Zitto.
Alisema kutokana na hali hiyo, ataendelea na shughuli za kamati yake kama kawaida.

MWANASHERIA WA ZITTO
Kwa upande wake, wakili wa Zitto, Alberto Msando, alisema hawezi kumshauri mwanasiasa huyo kijana kukata rufaa kwa kuwa Chadema wameonyesha kwamba hawamtaki.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha Clouds.
“Zitto huwa anapenda kufanya mambo yake akiwa huru, siyo kufanya shughuli zake za kitaifa huku akiwa anajua yeye ni mbunge kwa sababu ya mtu ama kitu fulani,” alisema.
Hata hivyo, alisema wameomba kupewa hukumu na taarifa ya mwenendo wa kesi yao, na watakapoipata na kuipitia watajua cha kufanya.
Akielezea hukumu kutolewa ilihali mlalamikaji akiwa hayupo mahakamani, Msando alisema walikuwa wakijiandaa kwenda mahakamani leo kusikiliza kutajwa kwa kesi hiyo na wala si uamuzi.
“Sisi tulikuwa tunajua kesho (leo) hii kesi ingetajwa, na pia tulijua kwamba jaji aliyekuwa na hii kesi amehamishwa, kwahiyo tulitarajia kwamba tungepangiwa jaji mwingine.
“Na siku hiyo walipokutana jaji aliandika kwamba sisi tujulishwe, lakini hakuna taarifa yoyote tuliyopata hadi tunakuja kuona taarifa ya hukumu kwenye mitandao,” alisema Msando.
Alisema kwa kawaida wakati wa kufungua kesi, huwa kuna sehemu ya kujaza mahala ambapo mhusika anaweza kupatikana endapo kuna taarifa anatakiwa kupewa na mahakama.

PROFESA KITILA
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Profesa Kitila Mkumbo, alisema hajashtushwa na hatua ya Chadema kumfukuza Zitto.
Profesa Kitila ambaye alifukuzwa uanachama wa Chadema akiwa pamoja Katibu Mkuu wa chama cha ACT, Samson Mwigamba kwa kosa la kuandaa uasi ndani ya chama mwaka 2013, alisema chuki ya chama hicho kwa Zitto ilikuwapo kwa muda mrefu.
“Hatua ya kumfukuza Zitto haijanishangaza kwani chuki ya viongozi wa Chadema dhidi ya Zitto ilikuwa kubwa. Kwanza Zitto alishafukuzwa tangu mwaka 2013,” alisema Profesa Kitila.

NEC YALONGA
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Julius Malaba, alisema bado hajapata taarifa ya maandishi ya kufukuzwa kwa Zitto, hivyo hawezi kuzungumzia.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kufanyika kwa uchaguzi mdogo kama jimbo hilo litabaki wazi, Malaba alisema kwa muda uliopo hakuna tena uchaguzi mdogo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles