28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ajali ya basi yaua 42 Iringa

WATU 42 wamefariki dunia na wengine 22 kujeruhiwa vibaya baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba mbao.
Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika eneo la Changalawe, Mafinga mkoani Iringa.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo aliiambia MTANZANIA kwamba basi hilo namba T438 CDE, mali ya Kampuni ya Majinjah Express lilikuwa likitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo basi hilo liligongana na lori hilo lililokuwa likitoka Iringa kuelekea Mbeya.
Alisema baada ya ajali hiyo abiria 37 walifariki dunia papo hapo na wengine watano walikufa baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.
Shuhuda huyo alisema ajali hiyo ilitokea lori lilipokuwa likikwepa mashimo yaliyopo eneo hilo na kwamba baada ya hatua hiyo lori hilo lilipoteza mwelekeo na kulilalia basi.
“Waliopoteza maisha walikuwa ni wanawake saba, wanaume 35 na watoto watatu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ambaye alifika eneo la tukio alisema ajali hiyo ni kati ya ajali mbaya ambazo aliwahi kuziona katika maisha yake.
“Ajali hiyo imesababishwa na mashimo yaliyopo hapo kwa sababu hata magari yanapishana kwa taabu wakati wa kukwepa mashimo hayo.
“Kutokana na ajali hiyo, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa imepiga kambi katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi kuhifadhi miili ya marehemu.
“Hata hivyo, miili 32 imesafirishwa hadi Haospitali ya Mkoa wa Iringa na miili mingine 10 itabaki katika hospitali ya wilaya hiyo kwa kuwa hospitali ya mkoa ina uwezo wa kuhifandi miili 32 na ile ya wilaya ina uwezo wa kuhifandhi miili saba,” alisema Masenza.
Naye dereva wa lori jingine, David Mosha, alisema aliona lori lililopata ajali likiyumba kutoka kulia kwenda kushoto upande lilipokuwa basi baada ya kupita kwenye shimo.
“Baada ya magari hayo kugongana, sikuweza kutoa msaada kwa sababu kontena la lori liliangukia basi na kulikandamiza. Jambo la ajabu ni kwamba mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja au miwili aliokotwa akiwa amelala chini ya basi akiwa hana majeraha.
Pamoja na hayo, aliilalamikia Serikali kwa kushindwa kujenga barabara hiyo kwa kuwa imeharibika muda mrefu.
Mmoja wa majeruhi aliyejitambulisha kwa jina la Musa Musega, alisema ajali hiyo ilisababishwa na mwendo kasi wa basi alilokuwa amepanda.
“Kabla ya ajali, tulimuita kondakta na kumuomba amwambie dereva apunguze mwendo kwa sababu alikuwa akiendesha kwa kasi.
“Tulipomwambia hivyo yule kondakta alituambia amemwambia dereva lakini hakutaka kumsikia,” alisema Musega.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Dk. Boaz Peter, alisema hospitali yake ilionekana kuzidiwa na majeruhi kwa kuwa hawajawahi kuhudumia majeruhi wengi kiasi hicho.
“Tumejitahidi kuwahudumia majeruhi wote na wale waliokuwa na hali mbaya tumewahamishia katika hospitali ya mkoa,” alisema Dk. Peter.
Baadhi ya marehemu walitambuliwa kuwa ni Ester Emanuel, Lusekelo, Jeremia Wakson, Dotto Katuga, Diga Solomoni, Teresia Kaminyonge, Frank Chiwangu, Luteni Sanga, Frank Mbaule, Mustapha Ramadhani, Shadrack Msigwa na Alferd Sanga.
Wengine ni Juliana Bukuku, Ester Fide, Paulina Justine, Catherine Mwajengo, Zera Kasambala, Rebeca Kasambala, Mbamba Ipyana, Dulile Kasambala, Mathias Justine, Christina Limo, Martine Haule na Dominic Mashauri.
Waliofariki dunia wengine ni Omega Mwakasege, Upendo Wiliam, Iman Mtange, Neto Sanga, Pili Vicent, Ester Wile, Lucy Mtenga, Erick Shitindi, Edwiga Kamyage, Frank Ndale, Kelvin Odubi na wengine walitambulika kwa jina moja moja la Hussen, Elias, Rafael, Musa na Osward.
JK atuma rambirambi
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kutokana na ajali hiyo mbaya.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kufuatia taarifa za vifo vya watu zaidi ya 40 huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika ajali hii mbaya ambayo imesababisha simanzi na majonzi makubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.

“Huu ni msiba mkubwa, na taifa kwa ujumla limepata pigo kubwa, hivyo naomba upokee salamu zangu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kutokana na ajali hii iliyotokea Mkoani kwako.

“Naomba, kupitia kwako, rambirambi zangu na pole nyingi ziwafikie watu wote waliopotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote mahala pema peponi, Amina,”alisema Rais Kikwete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles