25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

MATUMIZI MAKUBWA YASIYO YA LAZIMA HUANZIA KWENYE TABIA

placeholder-shopping

Na Christian Bwaya,

TUMEJARIBU kujadili tabia zinazoweza kukusaidia kutekeleza malengo yako. Tumeona kuwa utekelezaji wa malengo unayojipangia unategemea kwa kiasi kikubwa na vile unavyokuwa tayari kufanya mabadiliko ya msingi kitabia.

Tabia ndiyo msingi mkuu wa utekelezaji wa malengo. Unaposhindwa kubaini mchango wa tabia ulizonazo katika kukamilisha malengo unayojipangia, itakuwa vigumu kuyatekeleza.

Huwezi, kwa mfano, kuwa na lengo la kuongeza akiba unayojiwekea kila mwezi kwa kuendeleza mtindo ule ule wa maisha yasiyolingana na kipato. Matumizi makubwa yasiyo ya lazima yanaanzia kwenye tabia.

Moja wapo ya tabia ni kupenda kuwafurahisha wengine. Unapokuwa na shauku ya kuwafurahisha wengine utakuwa tayari kufanya matumizi yasiyo ya lazima. Utatoa michango na kuwakopesha marafiki kwa lengo la kuwafurahisha hata kama katika hali halisi uwezo wako wa kifedha hauruhusu. Unafanya matumizi kukidhi njaa uliyonayo ya kukubalika.

Kufanikiwa kwa lengo la kuongeza akiba, kunapaswa kwenda sambamba na kushughulikia mzizi wa tatizo ambalo kwa mukhtadha huu ni hamu ya kutamani kukubalika.

Hata hivyo, kubadili tabia si jambo jepesi. Tabia, kwa kawaida hujijenga kwa muda mrefu, hatua kwa hatua. Kupenda kuwafurahisha watu hakuji hivi hivi. Kunaanzia mbali. Tabia inapojijenga kwa muda mrefu, inakuwa sehemu ya wajihi wa mtu. Kama ilivyo vigumu mtu kubadili dini, ndivyo ilivyo unapotaka kubadili tabia iliyo sehemu ya utambulisho wa mtu.

Pamoja na hayo, bado tunaweza kubadili tabia zetu. Ili tuweze kubadili tabia tusizozipenda, tunashauriwa kufahamu mchango wa mambo madogo tunayoyafanya kila siku yanayotengeneza mambo makubwa tusiyoyataka.

Kama unachokifanya hakiendani na malengo uliyojiwekea, hata kama huoni athari yake leo, elewa kwamba unatengeneza mazingira ya kujikwamisha mwenyewe. Kufanikiwa kwa malengo yako kunategemea na vile unavyotambua mchango wa mambo yasiyoonekana kuwa na athari.

Nikupe mfano. Mtu anaweza kuwa na tatizo la kutokuwa mwaminifu kwenye ndoa yake. Kwamba hapendi kukosa uaminifu, mtu huyu anaamua kuweka lengo la kuachana na tabia hii. Kuweka lengo la kuacha uzinzi si kazi ngumu.

Utekelezaji wa lengo hili, hata hivyo, unategemea kwa kiasi kikubwa namna mtu huyu anavyotambua mchango wa vijitabia anavyovihalalisha kwa kisingizio kuwa havina athari yoyote kwenye maisha yake ya uaminifu.

Kuazimia kwa dhati kuacha uzinzi kutakuwa na maana kama kutaendana na kubadili mitazamo dhidi ya tabia hiyo. Maana yake ni kwamba ili mtu huyu afanikiwe, lazima akili yake isiruhusu kukubaliana na vitendo vya uzinzi hata kama vitendo hivyo havifanyiki katika hali halisi.

Kukubaliana na uzinzi usioufanya kunaweza kuwa sababu ya kuendelea na tabia hiyo. Kukosa uaminifu hakuanzi hivi hivi. Kunaanza na mtu kuwa na mtazamo chanya na vitendo hivyo hata kama havifanyi. Mtazamo chanya unajenga mazingira ya mtu kufanya kile ambacho ufahamu wake unachokiunga mkono tayari.

Ndio kusema ikiwa mtu analenga kuacha tabia hiyo, yampasa kuwa tayari kuachana na mazoea yasiyo ya lazima na watu wa jinsia yake. Kisaikolojia, anapofanya hivi, anapambana na mzizi wa tatizo, hatua inayoongeza uwezekano wa lengo husika kufanikiwa.

Ikiwa unatamani kubadilika, jifunze kuona mchango wa mambo madogo madogo ambayo wakati mwingine unajiruhusu kuyahalalisha. Mambo usiyoona athari yake kirahisi ndiyo yanayochangia kukwama kwa malengo yako.

 Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles