30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOMPELEKA MTOTO KITUO CHA MALEZI -2

10

Na Christian Bwaya,

MAKALA iliyopita tulizungumzia vigezo vitatu muhimu katika kuboresha huduma za malezi ya watoto vituoni, yaani day care. Tuliona kuwa ni muhimu idadi ya walezi (walimu) iendane na idadi ya watoto wanaonufaika na huduma inayotolewa. Pendekezo la jumla ni kuwa kituo kiwe na walezi wanaoweza kuwatazama watoto wachache kuwasaidia kujua mahitaji yao.

Pia tuliona ni muhimu walezi wawe na mafunzo maalumu ya makuzi na malezi ya watoto kuwawezesha kujua mahitaji mahususi ya watoto kulingana na umri. Changamoto ya kuwatumia walezi wasio na uelewa na makuzi ya mtoto ni pamoja na kuwa na matarajio makubwa kuliko uwezo wa watoto hali inayoweza kuwafanya watoto wajenge uadui na shule mapema.

Vile vile ili kuhakikisha kuwa walezi wanafanya kazi yao vyema, tuliona kuwa inashauriwa yakajengwa mazingira ya walezi kufanya kazi pamoja kwa vikundi vidogo.

Makala haya yanaangazia vigezo vingine vitatu vya kuzingatia unapofikiria huduma ya malezi ya kituoni.

Mazingira rafiki na salama kwa mtoto

Inashauriwa kituo kiwe na mazingira rafiki yanayomfanya mtoto ajisikie salama. Hiyo ina maana ya kuhakikisha kuwa walezi wanao uwezo wa kujenga mahusiano mazuri na watoto; hawabadiliki kila mara kwa lengo la kuwaondolewa watoto kadhia ya kukutana na sura ngeni mara kwa mara.

Pia, nyumba/jengo linalotumiwa kwa huduma ya malezi lisiruhusu mtoto kutoka bila uangalizi. Lengo ni kuhakikisha kuwa muda wote mtoto anabaki salama ndani ya jengo isipokuwa kwa uangalizi wa mlezi.

Usalama pia unakwenda sambamba na kupatikana kwa huduma bora za usafi na chakula, malazi safi, michezo na vifaa muhimu vya mtoto kujifunzia kulingana na umri.

Saa za mtoto kubaki kituoni

Tafiti nyingi zilizofanyika katika nchi zinazoendelea zinabainisha kuwa upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya muda mrefu anaoutumia mtoto kituoni na kuzorota kwa uhusiano wake na wazazi.

Kwa mfano; mtoto chini ya mwaka mmoja anapoachwa kwa zaidi ya saa sita kwa siku anaweza kujenga tabia hasi kama upweke na kukosa imani na wazazi. Ingawa hatuna tafiti zilizofanyika kwenye mazingira yetu, ni dhahiri kuwa upo umuhimu wa kupunguza muda wa kumwacha mtoto kituoni.

Hata hivyo, kadri mtoto anavyoendelea kukua, muda anaoweza kuachwa mtoto kituoni unaweza kuongezeka. Pamoja na hayo, ni vyema kuhakikisha kuwa mtoto anakaa muda mfupi iwezekanavyo kituoni sambamba na jitihada za kujenga uhusiano mzuri na mtoto mara baada ya kuondoka kituoni.

Hitimisho
Tunaweza kuhitimisha kuwa huduma hizi za malezi nje ya nyumba zetu, zinaweza kufaa. Jambo lililo muhimu kuzingatia ni ubora wa huduma zinazotolewa kwenye vituo hivi.

Katika jitihada za kuhakikisha kuwa vituo hivi vinaendeshwa kwa ubora, ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa vituo hivi vinasajiliwa. Wafanyabiashara wanaoanzisha huduma hizi walazimike kutumia majengo yenye ubora, wawe na vifaa muhimu vya michezo na waajiri walezi wenye mafunzo yanayotambuliwa.

Vile vile, tunahitaji sera za kazi za ajira zinazowezesha akina mama kufanya majukumu yao ya kimalezi bila changamoto kubwa. Kwa mfano, kuongeza muda wa likizo ya uzazi anayopewa mfanyakazi wa kike anayejifungua inaweza kusaidia kupunguza changamoto nyingi za malezi.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles