30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NCCR- Mageuzi kumteua Dk. Kahangwa urais 2015

George_KahangwaNA PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM
UMOJA wa Vijana wa Chama cha NCCR-Mageuzi, umempitisha Dk. George Kahangwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho ambaye atachuana na wagombea wengine watakaopitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Uamuzi wa kumpitisha mgombea huyo umekuja baada ya Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, kudai kuwa hatogombea tena nafasi hiyo kwa sababu anakwenda kugombea ubunge katika Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa vijana wa NCCR-Mageuzi, Deo Meck, alisema kikao kilichofanyika Machi 5, mwaka huu, kilifikia uamuzi huo baada ya kuona Dk. Kahangwa ana vigezo vya kuwania nafasi hiyo.
“Tulikaa kwenye vikao halali vya chama na kuamua kwa pamoja kupitisha jina la Dk. George Kahangwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, jambo ambalo limetufanya tuutangazie umma.
“Kutokana na hali hiyo, tutamuunga mkono mgombea wetu hata kwenye mchakato wa kupitisha jina la mgombea wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa sababu tunaamini ana vigezo vya kuongoza taifa hili,” alisema Meck.
Aliongeza kutokana na hali hiyo, wamewaomba wajumbe wengine kutoka Ukawa kuungana nao ili kuhakikisha mgombea huyo anachaguliwa kuwa mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Alisema Dk. Kahangwa amekuwa mwanachama wa chama hicho kwa miaka mingi, ni msomi wa kiwango cha juu na ana vipaji vingi visivyofungwa na mipaka ya taaluma yake.
Meck, alisema kutokana na hali hiyo, vijana hao wameamua kuchangishana waweze kumchukulia fomu ya kuwania nafasi hiyo katika ngazi husika ili aweze kupeperusha bendera ya chama ndani na nje ya nchi.

WASIFU WAKE
Dk. Kahangwa alizaliwa Mei 5, mwaka 1969 mkoani Kagera. Alipata elimu ya awali hadi ya sekondari katika shule mbalimbali hapa nchini.
Alipata Shahada ya awali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2004 ambapo alifaulu kwa kiwango cha juu kiasi cha kuibuka kuwa mwanafunzi bora wa kitivo.
Katika kipindi hicho, alikuwa mwanafunzi pekee aliyepata daraja la kwanza miongoni mwa wahitimu wa shahada ya BAED.
Mwaka huo huo alihitimu mafunzo ya uongozi katika taasisi ya Kijerumani ya Fredrich Ebert Stiftung (FES) ambako pia alikuwa mhitimu bora.
Mwaka 2007 alipata shahada ya pili (uzamili) katika chuo hicho na mwaka 2008 alisoma masomo ya elimu ya kimataifa katika Chuo cha Oulu nchini Finland.
Alimaliza shahada ya tatu (uzamivu) katika Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza mwaka 2013, ambako pia alitunukiwa shahada ya umahiri katika kufanya utafiti.
Andiko ambalo lilimpatia shahada hiyo lilihusu ujenzi wa uchumi wa maarifa kupitia sera ya vitendo katika elimu ya juu nchini Tanzania.
Kwa sasa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kampasi ya Mlimani, ambako anafanya kazi ya utafiti, kufundisha na kutoa huduma kwa jamii katika masuala ya uongozi, sera na mipango, hususan ya elimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles