Na ASHA BANI
ASKOFU Mkuu wa Makanisa ya Anglikana Tanzania Mhashamu Dk. Jacobe Chimeledya amemstaafisha kwa lazima Askofu Valentino Mokiwa kwa tuhuma za kuhusika na matumizi mabaya ya madaraka na mali za kanisa.
Askofu Mokiwa hadi anastaafishwa alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa barua kwa mapadri na maoskofu wote wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam ambayo MTANZANIA inayo nakala iliyoeleza sababu za kufukuzwa kwake kuanzia juzi Januari 7, mwaka huu na kwamba sio tena askofu wa makanisa hayo.
Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi iliyoundwa kwa ajili ya kumchunguza Mokiwa, Sylivester Haule alisema kiongozi huyo alilazimishwa kuvuliwa uaskofu huo ambapo awali alikaidi.
Haule ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Mtakatifu Andrea lililopo Magomeni Jijini Dar es Salaam, alithibitisha kuvuliwa kwa uaskofu wa Valentino Mokiwa.
Alisema sababu za kuvuliwa madaraka kwa kiongozi huyo wa muda mrefu wa kanisa hilo ni kudaiwa kuhusika kwake na ufujaji wa mali za kanisa na matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema hatua hiyo inatokana na mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake na wadhamini wa makanisa mbalimbali ya jimbo la Dar es Salaam, ambayo ni Yombo Buza na Magomeni ambayo walilalamikia hatua ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kile walichoita ufisadi huku wakimtaka aandike barua mwenyewe ya kujiuzulu lakini aligoma kufanya hivyo.
Alisema Mokiwa alikuwa akikabiliwa na mashtaka 10 ambapo shtaka la tatu la uwekezaji ndiyo lililomtia hatiani na yeye kukiri kosa mbele ya tume hiyo ya uchunguzi.
“Katika shtaka namba tatu lilikuwa ni pamoja na kufuja mali za kanisa ikiwa ni pamoja na ekari 400 zilizopo kanisa la Buza alimega ekari 200 na kumpa mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina la Kishimba huku kanisa likiwa halina taarifa.
“Pi a wadhamini walimlalamikia lakini hakuweza kusikia huku akiendelea kuuza na kugawa mali zingine za kanisa kinyemela kinyume na makubaliano ya vikao na utaratibu wa kanisa,” alisema Haule
Mwenyekiti huyo wa Tume ya Uchunguzi, alisema kuwa eneo lingine ambalo liliingia katika kosa namba tatu ni la Benki ya Wanachi Dar es Salaam (DCB), ambayo makubaliano ya awali wawekezaji hao walitakiwa kufanya ujenzi kulipa Sh bilioni 5 kisha kuwa mali ya Kanisa lakini Mokiwa aliandikisha kwa Sh bilioni mbili na baada ya mkataba kuisha Mokiwa aliwatetea wawekezaji hao.
“Unajua ilikuwa ni kama aina fulani ya ufisadi maana makubaliano na waliojenga ilikuwa walipe Shilingi bilioni tano walivyotugeuka Askofu Mokiwa anatetea naye na kusema kuwa ni Shilingi bilioni mbili jambo ambalo si sahihi,’’ alisema
“Baada ya yote hayo kubainika Askofu Mokiwa hakukanusha alikiri makosa lakini alitakiwa kujiondoa yeye mwenyewe kwa kuandika barua ya kujiuzulu siku ya Desemba 7, mwaka jana ila alikaidi pia huku akiendelea na kazi zake mpaka hapo alipovuliwa kwa lazima,’’alisema Haule.
Aliongeza kuwa baada ya kukaidi maaskofu wakuu walikutana kwa ajili ya kujadili suala hilo kuanzia Desemba 21 hadi 24 na baada ya hapo maamuzi yakatolewa Januari 7 kwa kuamua kuwa si Askofu tena.
Aliongeza kuwa Askoafu Mokiwa kwa sasa anatakiwa kukabidhi ofisi za kanisa na kufanyiwa ukaguzi wa hesabu.
Mwandishi alipomtafuta Askofu Mokiwa ili kuzungumzia taarifa za kuvuliwa kwake madaraka, simu yake ya mkononi haikupatikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.