23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA KUUMANA VIKALI KESHO

*Ni nusu fainali Kombe la Mapinduzi


simba-na-yangaNa MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

VIGOGO wa soka nchini Simba na Yanga, kesho wataumana vikali katika pambano la kukata na shoka kwenye hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kumalizika Januari 12, mwaka huu.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya Simba kufanikiwa kuongoza Kundi B kwa kufikisha pointi 10 kutokana na ushindi wa mabao 2-0 waliopata jana dhidi ya Jang’ombe Boys.

Kundi la Simba lilikuwa na ushindani mkubwa lakini Wekundu hao wa Msimbazi tayari wamejihakikishia tiketi ya kutinga nusu fainali ambapo sasa watakutana na watani wao wa jadi Yanga wanaoshika nafasi ya pili Kundi A.

Kwa mara ya mwisho Simba na Yanga zilikutana Oktoba mosi mwaka jana katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa matokeo ya sare ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Simba na Yanga kukutana tangu timu hizo zilipofanya usajili kwenye dirisha dogo ili kuimarisha vikosi vyao.

Yanga waliofanya mabadiliko ya benchi lao la ufundi, watavaana na Simba katika pambano hilo wakiwa chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina ambaye atakutana uso kwa uso na mahasimu wao kwa mara ya kwanza tangu aanze kibarua cha kuifundisha.

Yanga wamepangwa kukutana na mahasimu wao Simba kutokana na kushika nafasi ya pili katika Kundi B baada ya kipigo cha mabao 4-0 walichokipata juzi dhidi ya Azam FC.

Katika mchezo wa jana mabao ya Simba yalifungwa na mshambuliaji, Laudit Mavugo ambaye ameibuka kwa kishindo baada ya kushindwa kuonyesha makali yake katika mechi za Ligi Kuu.

Mavugo aliifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 11 ya mchezo baada ya kupiga shuti lililojaa wavuni akiunganisha pasi safi ya Shiza Kichuya.

Bao hilo liliwaongezea kasi Simba ambapo dakika ya 17, Kichuya akiwa ndani ya eneo la hatari alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuitumia vyema pasi ya Mavugo.

Dakika ya 20, Jang’ombe Boys walifanya shambulizi kali langoni kwa Simba lakini shuti lililopigwa na Khamis Makame akiwa ndani ya eneo la 18 akiunganisha pasi ya Ibrahim Said, halikuzaa matunda.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Simba wakitawala mchezo kwa asilimia kubwa, ambapo dakika ya 52, Mavugo aliandika bao la pili baada ya kupiga shuti la mbali ambalo lilitinga moja kwa moja wavuni akiunganisha pasi ya Kichuya.

Hata hivyo, baada ya kufunga bao la pili, kocha wa Simba Mcameroon, Joseph Omog, alimpumzisha Mavugo  na nafasi yake kuchukuliwa na Jamal Mnyate.

Baada ya kufungwa mabao hayo, Jang’ombe Boys walicharuka na kuanza kulishambulia lango la Simba bila mafanikio kutokana na kipa Manyika Peter kuwa imara katika kuokoa hatari zilizokuwa zikielekezwa langoni mwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles