29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KWANINI UCHAWI WETU HAUJENGI VIWANDA

Waziri mkuu Kassim Majaliwa atembelea kiwanda cha kushona nguo cha Tooku jijini Dar
Waziri mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea kiwanda cha kushona nguo cha Tooku jijini Dar es Salaam

NA MARKUS MPANGALA,

KATIKA jamii ya Kitanzania suala la uchawi ni miongoni mwa mambo yanayojadiliwa, kuheshimiwa na kuaminiwa na baadhi yao. Labda tupate tafsiri ya uchawi ili tuweze kuelewana vema katika hoja yetu ya leo.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la 3, neno ‘uchawi’ limeelezwa kwa namna mbili; Mosi ni ufundi wa kutumia dawa au vitabu maalumu vya uganga ili kuleta madhara kwa viumbe; au juju. Pili ni vifaa vinavyotumika katika shughuli za kurogea.

Kwamba mwanadamu yeyote anayedaiwa kuwa mchawi ametafsiriwa kuwa ni mtu anayeweza kuwadhuru watu kwa kuwaroga; mlozi, kahini. Kamusi ya Merriam-Webster imetoa maana ya uchawi (witchcraft)  kwamba ni mambo ya kimiujiza yanayofanywa na wachawi.

Aidha, kamusi hiyo inaeleza matumizi ya nguvu za kiroho zilizochukuliwa toka kwa roho waovu. Wengine wanatafsiri uchawi kama matumizi ya silaha za mashetani au nguvu za mashetani ili kusababisha madhara kwa watu.

Kimsingi wapo Watanzania wanaoamini uchawi ndiyo njia yao ya kuishi vizuri. Wengine huamini watafanikiwa kwenye biashara, kazini na shughuli mbalimbali za kiuchumi, siasa na jamii.

Habari za uchawi ni nyingi na kwa baadhi yetu tuliokulia vijijini katika mikoa mbalimbali tunaamini kuwa uchawi upo na wengine tumeushuhudia.

Rafiki yangu ambaye ni mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW), Mohammed Ghassani, anakiri kuwahoji watu mbalimbali juu ya dhana ya uchawi na kwamba hiyo ni sayansi pekee ambayo Mzungu ameshindwa kuitumia. Anasema dhana hiyo ipo na inafanya kazi kwa watu wanaoamini.

Hata hivyo, huko barani Ulaya dhana ya uchawi ilipata kuchukua nafasi katika nyakati nyeusi (ambazo zilitawaliwa na elimu duni). Uthibitisho wa kusambaa wachawi huko barani Ulaya unatolewa kwenye kitabu cha “Witch hunts in western world” kilichoandikwa na Brian A. Pavlac. Kwamba wachawi walichomwa moto, walishtakiwa, walitengwa na kufanyiwa mabaya ya kila namna.

Sasa basi, kwa kuwa dhana ya uchawi inatajwa kama miongoni mwa sayansi bora zaidi katika dunia hii inayopatikana zaidi barani Afrika, ikiwemo Tanzania, yatupasa kujiuliza manufaa ya uchawi wetu. Kuna uchawi unaotajwa kufanywa kwa kafara kwenye shughuli za biashara, kazini na mengineyo. Sina hakika juu ya masuala hayo lakini ukweli ni kwamba hapa Tanzania mambo ya uchawi yametamalaki kila kona.

Swali langu kwa wasomaji wa safu hii, hivi kama uchawi ni sayansi iliyomshinda Mzungu na ambayo inapatikana zaidi Afrika je, ni kwanini tusitumie kama nyenzo ya kujenga viwanda, kuvutia wawekezaji, watalii, ujenzi wa barabara, majengo na makampuni yenye nguvu kibiashara hapa nchini?

Kwanini kama uchawi huo una malengo mazuri na wenye tija kwa jamii unangojea nini kutuletea mafanikio ya kujenga viwanda, utajiri wenye mashiko kwa wananchi? Ni kwa vipi tumeshindwa kuufanya uchawi huo utuletee viwanda vya magari ya aina mbalimbali.

Kwanini uchawi usituletee barabara za lami kila kona ya nchi hii? Kwanini tushindwe kuwa na mafanikio ya kiuchumi hadi tuitwe nchi masikini kama uchawi ndiyo nyenzo ya kuwa na uchumi wa viwango vya Marekani na nchi nyinginezo za Ulaya na kadhalika.

Ikumbukwe hapa sizungumzii utajiri wa kiroho ambao unajazwa maneno na imani ya Mungu. Vile vile imani ya Mungu si umasikini, njaa, utapiamlo na magonjwa yanayotibika lakini tunakimbilia kwenye maombi kwa kisingizio kuwa ndio njia pekee. Kwanini tusifike mahali tukaona uchawi huo utusaidie kutwaa Kombe la Dunia, Afrika katika ngazi za klabu au timu za taifa.

Kwanini uchawi huo usituondolee mapigano ya wafugaji na wakulima? Kwanini uchawi huo usitusaidie kujenga mahoteli, vituo vya mafuta, maduka ya kisasa maarufu kama supamaketi? Kwanini tushindwe kuleta mafanikio ya uchumi badala yake tumekazania kuwadhuru ndugu, jamaa na marafiki?

Nakumbuka tukio moja lililotokea huko Ghana. Mwanamke mmoja alikuwa akiishi Marekani, kila mara alikuwa akituma fedha ili ajengewe nyumba yake. Ndugu waliokuwa wakisimamia walimwahidi usimamizi na kumwambia maendeleo ya ujenzi wa nyumba yake huko kijijini.

Nyuma ya pazia hapakuwa na ujenzi wowote na yule ndugu yao alipoahidi kutembelea nyumba yake huko Ghana  baada ya kufika uwanja wa ndege nchini humo akapatwa na wazimu. Mwingine tumehabarishwa hivi karibuni kwenye sherehe za Krismasi 2016.

Jamaa mmoja na mkewe walikwenda kwa kaka yake mara baada ya kufika kutoka ughaibuni wakiwa na lengo la kusherehekea kwa ndugu huyo kabla ya kuelekea kwao. Cha ajabu wakawekewa sumu na kupoteza maisha.

Hivi kama uchawi una manufaa sana kwanini tumebaki masikini? Kwanini tuendelee kuitwa taifa masikini ilhali jamii yetu inahusudu uchawi usitujengee viwanda? Na umasikini si sifa nzuri ya jamii inayojitambua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles