Na JUDITH NYANGE – MWANZA
MWEKEZAJI wa kiwanda cha kusindika nyama cha Chobo Investment Co Ltd kilichopo Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza, amelalamikia tatizo la ardhi ya kufikisha mifugo inayotumika kama malighafi kiwandani hapo.
Akizungumzia changamoto zinazomkabili katika uwekezaji wake juzi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mkurugenzi wa Chobo Investment Co Ltd, John Chobo, alisema anakabiliwa na changamoto kubwa ya kupata ardhi ya kupitisha mifugo 1,520 ili kufikia malengo ya uzalishaji wa kiwanda hicho.
“Sehemu pekee tunayoweza kupata ardhi ni halmashauri, tulishapeleka maombi yetu wizarani miaka miwili iliyopita mpaka sasa hatujajibiwa wala kupata ufumbuzi wowote, hali hii inasababisha gharama zetu za uendeshaji ziwe kubwa kwani tunalazimika kutafuta eneo jingine na kulilipia kwa ajili ya kuhifadhi mifugo hiyo,” alisema Chobo.
Alisema katika eneo hilo, wanakabiliwa na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara pamoja na maji ambapo wanalazimika kutumia Sh milioni 12 kuagiza kila mwezi kununua maji kwenye matanki ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa).
Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Mwauwasa, Mhandisi Manyama Manyama, alisema kutokana na changamoto zilizopo Wilaya ya Misungwi, wanafanya utafiti eneo la Usagara kuangalia uwezekano wa kufikisha miundombinu ya maji katika eneo hilo na kuliweka katika bajeti ya mwaka 2017/18.
Alisema gharama zilizoainishwa zinafikia Sh bilioni 3.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Leon Matata, alisema tatizo la kukatika kwa umeme litakwisha baada ya kukamilika laini ya umeme ya kilovoti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga na laini ya kilovoti 220 kutoka Bulyanhulu hadi Geita, itakayopunguza changamoto katika laini ya Sengerema hadi Geita iliyokuwa na hitilafu mara kwa mara.
Naye Mongella alisema ni lazima matatizo yaliyopo katika viwanda hivyo kwa sasa yashughulikiwe kwa wakati kwa sababu haiwezekani wakahamasisha kuanzishwa viwanda vipya na vile vya zamani vikafa au kudorora, hali hiyo haitakuwa na maana katika kuvutia uwekezaji.