Na ESTHER MNYIKA-DAR ES SALAAM
SERIKALI bado inaendelea na ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege 11 katika mikoa mbalimbali, ikiwa ni mpango wake mkakati wa kuboresha na kukuza usafiri wa anga hapa nchini.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, Serikali ilitenga Sh bilioni 100 kwa ajili ya kutengeneza na kukarabati viwanja vya ndege kwa kiwango cha lami.
Ukarabati na upanuzi wa viwanja hivyo ni mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi wa viwanja hivyo unaboreshwa na kuwa wa kisasa kwa kiwango cha kimataifa, ili kuwezesha ndege kubwa kutua kwa wingi na salama wakati wote katika viwanja hivyo.
Matengenezo hayo ni ya gharama kubwa na hivyo basi itakuwa ni busara kama wasimamizi na watumiaji wa viwanja hivyo watavilinda na kuvitunza mara baada ya matengenezo hayo.
Lakini pamoja na utunzaji wake, kuna haja ya Serikali yenyewe kuvitangaza viwanja hivyo ili viweze kuwavutia watumiaji wengi, wakiwamo watalii kutoka nchi mbalimbali, ili iweze kuingiza fedha nyingi za kigeni na kuongeza pato la taifa.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za taarifa zilizopo, upanuzi wa uwanja wa Dodoma umegharimu Sh biloni 11.5 kutoka kwenye bajeti ya Sh bilioni 100 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati katika kiwango cha lami.
Uwanja wa Ndege wa Mwanza umegharimu Sh bilioni 105 na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam Terminal 2 umegharimu Sh bilioni 600 na walitegemea fedha hizo za bajeti zitengeneza viwanja vinane, hivyo kuleta sintofahamu kwa Serikali.
Kwa hatua hiyo, Uwanja wa Ndege wa Mwanza utakuwa kiungo muhimu katika mikoa kumi ya Kanda ya Ziwa na Kati katika usafiri wa anga.
Tunazungumzia uchumi wa viwanda ambapo Serikali imeweka mikakati na vitegauchumi mbalimbali boresha taasisi, ikiwamo viwanja vya ndege ili kufikia malengo.
Serikali ikiwa safi kwa mpango mkakati itasadia kuinua uchumi mbalimbali kupitia viwanja na kwa vile maendeleo yataongeza na kuinua hali ya uchumi wa watu, matumizi ya ndege ndiyo sahihi, kwani wataalamu hawapendi kupoteza muda.
Serikali imeongeza ndege na hivyo viwanja ni sehemu muhimu ya mkakati huo.
Katika juhudi za kufufua Shirika la Ndege nchini (ATCL) inategemea kutawala soko la usafiri wa anga la Tanzania na kushindana vilivyo na Precision Air na Fast Jet.
Serikali itanunua ndege 4, zikiwamo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini wanaotoka hasa nchi za Ulaya na Marekani.
Hivi karibuni, Rais Magufuli akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Ikulu Dar es Salaam, aliahidi ununuzi wa ndege hizo ambapo alisema alishalipia asilimia 30 na zinatarajiwa kufika nchini mwanzoni mwa mwaka 2018.
Ununuzi huo wa ndege mpya umetajwa kufanyika kwa wakati mwafaka, wakati washindani katika biashara ya usafiri wa anga, Precision Air na Fastjet, wakitangaza kupata hasara na kupunguza safari za baadhi ya miji, huku hatua za kuahirisha safari zikichukuliwa mara kwa mara.
Hali hiyo inaashiria kupungua kwa huduma na hivyo kuongezeka usumbufu kwa wananchi na jawabu lake ni kwa Serikali kuwa na ndege zake kuendelea kutoa huduma nchini kote.
Wiki iliyopita Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha Mwanza,
Mbarawa anasema ni kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 150 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya upanuzi wa viwanja ambavyo baadhi ni vya Shinyanga, Tabora, Sumbawanga, Kigoma, Mtwara, Songea na Iringa.
Anasema kuwa, miradi itakayotekelezwa katika viwanja hivyo ni pamoja na ujenzi wa majengo ya abiria na upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege.
“Maboresho ya miundombinu ya viwanja vya ndege yatachochea ongezeko la pato la Taifa, hivyo basi Serikali imeonesha nia ya dhati katika kuhakikisha usafiri huu utakuwa ni wa uhakika na nafuu kwa wananchi,” anasema Profesa Mbarawa.
Kuhusu ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, Profesa Mbarawa anasema Serikali imeshatoa Sh bilioni 7.6 kwa ajili ya kumlipa mkandarasi na msimamizi wa mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika Agosti mwakani.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), Salum Msangi, ameahidi kuendelea kutatua changamoto ya ndege hai ambao mara kwa mara wamekuwa na uharibifu wa miundombinu, hasa katika injini za ndege katika uwanja huo na hivyo kuhatarisha usalama wa anga na watumiaji wake.
Mjenzi wa jengo hilo ambaye ni Mkandarasi wa Kampuni ya Beijing Engineering Construction Group (BECG), Yuzhang Xiong, amemhakikishia Waziri huyo kukamilisha ujenzi huo kwa wakati, kwani kwa sasa jengo limefika katika hatua nzuri.