27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: MADINI VIWANDA YATASISIMUA UCHUMI

viwanda
Dolomite ikichimbwa na kusafirishwa kwenda kiwandani

 

Na SHERMARX NGAHEMERA,

KUNA mapinduzi makubwa katika uchumi wa Tanzania unaoendelea kukua na kudai mambo mapya, kwani mahitaji yamebadilika.

Sera ya Serikali ya kutaka uchumi wa viwanda imeamsha mahitaji mapya kwenye sekta ya madini ambayo hapo awali madini viwanda hakuna, mtu alikuwa anayajali lakini sasa hali imebadilika na wawekezaji wengi wanayatafuta kama rasilimali kwa ajili ya malighafi ya viwanda vyao.

Madini ya chokaa, udongo mfinyanzi, kaolin, magnesite, rare earth, dolomite, jasi, fosfeti, grafaita na chuma yanatafutwa kwa ajili ya uwekezaji, kitu ambacho awali hakikuwapo na watu awali walikuwa wakitafuta madini mkakati ya koltani, urani, dhahabu na shaba.

Madini mengine Tanzania ya viwanda ni diatomite, bentonite, vermiculite, chumvi, mchanga pwani, udongo mfinyanzi, bati, wolfram, dolomite, manganese, uno na kaolin.

Madini hayo yametapakaa nchi nzima na hivyo kutoa chachu kwa wawekezaji kuwa wasiwe na wasiwasi, kwani malighafi ya kufanyia kazi imesheheni nchini.

Mambo mapya hudai mahitaji mapya na kila  siku uchumi wa Tanzania utazidi kuimarika kama tutachukua maamuzi sahihi juu ya uchumi huo na namna ya kuuendesha hatua kwa hatua.

Serikali awamu ya Tano kimwenendo imekuwa kaidi na kutoa kipaumbele kwa kusisitiza kuwa madini ya hapa nchini yatumike na viwanda vya nchini ili kuyaongeza thamani na hivyo kutoa ajira na vilevile kufanya viwanda vya hapa nchini viwe shindani zaidi kwa kutumia rasilimali za ndani na hivyo kutoa mazao ya bei ya chini. Ni mtazamo mzuri wa kujitegemea.

Alhaj Aliko Dangote wa Dangote Industries Group na bilionea namba moja Afrika anasema yeye akienda kuwekeza kwa kujenga kiwanda mahali fulani kama alivyofanya Tanzania basi atatumia malighafi ya pale nchini ili kufanya gharama za uzalishaji ziwe za chini na hivyo kuwa shindani sokoni.

Dangote alitofautiana na wataalamu wake ambao walizuga wanataka kuagiza makaa ya mawe, jasi na gesi kutoka nje kwa madai mazao ya hapa hayafai. Alikataa na kusema mazao hayo ni bora kuliko na hivyo aliwataka wabadili mtazamo wao wa kilanguzi.

Kwa Tanzania kuamua kutumia jasi na makaa ya mawe kutoka nchini, ni uamuzi uliochelewa sana, kwani kwa muda mrefu ulitakiwa kufanywa, lakini vikazuka visingizio chungu mzima na  wenye viwanda kuzuia kutekeleza uamuzi huo wenye tija kwa nchi na watu wake. Lakini imefikia ukomo.

Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini ni msomi aliyebobea wa masuala ya madini, amegundua  hujuma na ghiliba inayofanyika kwa nchi na amefanya uamuzi sahihi kwa kusimama kidete kutetea matumizi ya madini viwanda yaliyoshamiri nchini. Anauliza kama sisi wenyewe hatuyatumii nani atafanya hivyo? Baada ya miaka mitano nchi itabadilika vilivyo.

Ukweli ni kuwa ni madini viwanda na siyo vito na dhahabu ambacho huinua haraka uchumi wa nchi kutokana na wingi na uhakika wake na urahisi wa kuyachimba madini hayo kwa kuwa yanakuwa katika mfumo wa  tabaka katika mwamba.

Mfano mwafaka na rahisi ni kuwa bei ya maji ni kubwa kuliko ya mafuta, lakini upatikanaji wake ni kidogo na rahisi, lakini wingi wa mafuta na mahitaji yake unaofanyiwa biashara hufanya nchi zenye mafuta ziwe tajiri kupita wenye maji. Kuna matumizi lukuki ya mafuta na si maji na hivyo kufanya nishati hiyo iwe na thamani kubwa machoni mwa watu, lakini tunakoendelea maji yatayapiku mafuta kama kimiminika, kwani ni uhai.

Kiuchumi Marekani kwa Japan ni nchi ya Dunia ya Tatu, kwani Marekani inauza sana madini viwanda kwake, wakati Japan inaiuzia  bidhaa za viwandani na za teknolojia ya juu.

Serikali imezuia kuagiza jasi na makaa ya mawe kutoka nje kuja kutumika kama malighafi ya viwanda vyetu, kwani Tanzania kama  nchi ina rasilimali ya kutosha na ya ziada kwa  mahitaji ya nchi. Dangote naye amethibitisha ukweli huo wa Serikali.

Msimamo wa Serikali ulitolewa baada  ya vikao viwili kati ya Wizara na wadau ambao ni wachimbaji wa madini, wenye viwanda na Serikali, kila upande kueleza mahitaji, ubora  na matumizi pamoja na kiwango cha uzalishaji.

Waziri Muhongo aliwataka kila mmoja aeleze mahitaji na shida za utendaji, halafu katika mkutano wa pili uwe msingi wa majadiliano.

Kwenye kikao cha pili Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, alitoa azimio la Serikali la kuzuia uingizaji madini hayo kutoka nje, kwani uzalishaji wa ndani unatosheleza.

Dk Kalemani alibainisha kuwa, uzalishaji nchini ni tani 354,000 na mahitaji ya soko ni tani 30,000 kwa mwezi katika viwanda vya saruji nchini. Kwa makaa  ya mawe uzalishaji ni tani 50,000 kwa mwezi na mahitaji ni tani 30,000 kwa mwezi, huku akiba ya nchi ikiwa tani milioni tano  na hivyo kuwa ni ya uhakika kwa zaidi ya miaka 150 ijayo.

Viwanda vingi vina kasumba na wakipewa maagizo hawataki kutekeleza na hivyo kuleta lawama zisizo na msingi. Mazoea ya chajuu yana tabu sana!

Kinachoendelea sasa ni kuzusha kuwa wakielezwa watengenezaji makaa ya mawe hawazalishi kufuatia vigezo vya mahitaji, lakini wakiambiwa walete uthibitisho inakuwa muhali kwao.

Jasi iliyokuwa inatumika viwandani inatoka Afrika Kusini na Zimbabwe, wakati nchi ina rasilimali ya kutosha kutoka kule Makanya, Lindi, Itigi na Simiyu. Jasi hiyo ni ya ubora wa hali ya juu na nyingine kufikia kiwango cha ubora wa asilimia 98. Jasi ya Lindi ina ubora wa asilimia 99.

Makaa ya mawe yako mikoa mingi ya Tanzania, lakini mengi sana ni yale kutoka Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Sumbawanga, Katavi, Mbeya, Njombe na Ruvuma.

Miradi ya makaa ya mawe

Mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa  na Njombe  ndiko kwenye miradi mingi na mikubwa ya makaa ya mawe, mingi ikilenga kuzalisha umeme, sasa inatakiwa ibadilike ili kutumia fursa iliyojitokeza ya kuwa malighafi ya kutengeneza saruji au kupashia joto baada ya Serikali kupiga marafuku uagizaji kutoka nje.

Wizara ya Madini imethibitisha na kusema kuwa Tanzania ina kiasi cha tani bilioni tano na kurekebisha ile hesabu ya zamani ya tani bilioni 1.5 kufuatia uvumbuzi wa hazina nyingine.

Chanzo kingine cha makaa ya mawe ni mradi wa kule Ludewa, ambapo Kampuni ya Kichina, China Sichuan Hongda ina mradi na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) wa dola za Marekani bilioni 3 kuchimba chuma na makaa ya mawe, lakini maendeleo ya mradi ni goigoi.

Mradi mwingine mkubwa ni ule wa Kiwira, ambao unaendeshwa  na Shirika la Taifa la Madini (Stamico) ambao una matatizo ya uongozi na mtaji kiasi kwamba unasuasua na haueleweki.

Viwanda Mkoa wa Pwani

Viwanda vinavyojengwa 40 Mkoa wa Pwani kama vikianza kazi vitatumia malighafi toka nchini, ikiwamo makaa ya mawe, chuma ghafi, kaolini, uno, chokaa, dolomite, mchanga pwani, udongo wa mfinyanzi, jasi na mengine na hivyo kuongeza mahitaji ya madini hayo katika soko.

Ukiachia jasi, wachunguzi wa mambo ya madini wana wasiwasi uwezo wa nchi kuchimba makaa ya mawe, kwani imedhihirika kwa muda mrefu kuwa ni miradi ya makaratasi zaidi kuliko uzalishaji na hivyo kuitaka Serikali isiingie mkenge na kusitisha uagizaji mpaka ijiridhishe yenyewe, vinginevyo nchi itaangamia na kusimamisha uzalishaji saruji.

Serikali inatakiwa kuunga mkono wazalishaji wa jasi pale Makanya, Wilaya ya Same, ili kuongeza uzalishaji na kufanya ufufuaji wa reli ya huko inayokwenda Arusha, Moshi na Tanga kutoka Ruvu iwe na tija. Hata migodi ya dhahabu nayo huhitaji jasi na chokaa.

Pamoja na hilo, viwanda vya simenti vilazimishwe kuzalisha saruji mpaka kufikia kikomo, kwani wazalishaji wengi uzalishaji wao ni chini ya asilimia 50 ya uwezo wa kiwanda na hivyo kufanya nchi itambae wakati ingeweza kukimbia. Katika ujenzi hakuna mbadala wa saruji.

John Massawe anasema yeye aliwahi kufanya Saruji Corporation enzi hizo na anasema ripoti ni kuwa kwa kiwanda kimoja uzalishaji umeendelea kuwa duni, ingawa kwa ujumla umeongezeka.

 Anasema kama nchi, “Tusifanye makosa”.

Wakati mwingine Serikali hufanya makosa ya kusaini mikataba ya viwanda na kusema kuwa malighafi itoke nje. Si vema, kwani kufanya hivyo ni kudumaza maendeleo ya viwanda na uchumi wetu. Lazima tulazimishe kuwa malighafi itoke nchini, kwani mwishowe itakuwa rahisi na kuwa na uhakika nayo na hivyo kuwa shindani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles