KINSHASA, DRC
WATU 22 wameuawa kikatili katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa mujibu wa maofisa wa jimbo hilo juzi.
Vifo hivi ni vya hivi karibuni katika wimbi la miaka miwili ya ghasia katika jimbo hilo.
Mauaji hayo yametokea katika mji wa Eringeti, uliopo kilomita 55 kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Beni.
Mji huo umekuwa ukikumbwa na mlolongo wa mashambulio ambayo tayari yamesababisha vifo vya raia 700, kwa mujibu wa ofisa wa mkoa huo, Amisi Kalonda, ambaye amewalaumu waasi kutoka Uganda kwa mashambulio ya hivi karibuni.
Kalonda amesema wajumbe wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi lenye idadi kubwa ya Waislamu wenye itikadi kali kutoka Uganda ambao wamekuwa kwenye ukanda huo kwa zaidi ya miongo miwili, walivamia mji huo Jumamosi mchana.
“ADF wamewashambulia tena wakazi wa Eringeti na maeneo yanayozunguka mji huo asubuhi,” aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kutoka mji mkuu wa Kivu Kusini wa Goma.
“Jana (Jumamosi), waliwaua raia 10. Miili mingine ya watu 12 ilipatikana leo Jumapili katika vijiji vinavyozingira mji,” alisema Kalonda akiongeza kuwa waathirika waliuawa kwa visu na mapanga.
Kwa miaka miwili iliyopita eneo linalozingira mji wa Beni limekuwa likikumbwa na mauaji ya kikatili yaliyoua mamia ya raia, wengi wao wakichinjwa na kunyongwa hadi kufa.
Msemaji wa Jeshi la Kongo, Mak Hazukay amethibitisha kutokea kwa shambulio hilo, akisema wanajeshi waliwaua waasi wa ADF, lakini akiongeza kuwa idadi ya raia waliokufa ni kubwa.
Maafisa wa Kongo wamekuwa wakiwalaumu waasi wa ADF kwa mauaji hayo, lakini ripoti kadhaa za wataalamu zimekuwa zikisema makundi mengine, ikiwamo vikosi vya serikali huhusika katika baadhi ya mauaji.