NA CLARA MATIMO- MWANZA
KUKOSEKANA kwa tiba ya ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi katika hospitali za mikoa kumetajwa kuwa ni changamoto kubwa inayowakabili watu wenye ugonjwa huo hapa nchini.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi Wenye Watoto wa Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi Tanzania (ASBAHT) Mkoa wa Mwanza, Elias Ntale, alipozungumza na MTANZANIA kuhusu changamoto ambazo wanakumbana nazo kuwahudumia watoto wao wenye ugonjwa huo.
Alisema ili mtoto mwenye ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi aweze kupatiwa matibabu, ni lazima mzazi asafiri naye hadi mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro na Dar es Salaam kupata tiba katika hospitali za taifa za rufaa ambazo ni Bugando, Kilimanjaro na Muhimbili ambako ndiko madaktari wanapopatikana.
Alisema matibabu hayo hutolewa kwenye hospitali zilizopo mikoani pale wafadhili wanapopatikana tu na hutokea mara chache kutegemea na neema inayowashukia wagojwa waliopo katika mikoa hiyo.
“ASBAHT tuna imani sana na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa nia ya rais wetu ni kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za matibabu, naomba tusaidiwe ili huduma za matibabu kwa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi ziwe zinatolewa katika hospitali za rufaa za mikoa.
“Sisi wazazi tunaelewa kwamba kuna uhaba wa madaktari bingwa hapa nchini, lakini tunaiomba Serikali itusaidie angalau kila baada ya miezi mitatu huduma hii itolewe mikoani maana watoto wengi wanachelewa kupatiwa matibabu kutokana na wazazi wao kukosa gharama za usafiri na umbali wa kufika hospitalini,” alisema Ntale.