Na Ramadhan Libenanga-Morogoro.
NI ukatili wa kutisha. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mtu mmoja kunusurika kifo, baada ya kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea nyuma ya shingo.
Mbali na ukatili huo, watu wengine wanane wamejeruhiwa vibaya na kulazwa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea Kijiji cha Dodoma Isanga juzi.
Mapigano hayo yamekuja siku mbili baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, kuonya juu ya Taifa kunyemelewa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.
Alisema hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje kama njugu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mkulima wa kijiji hicho, Stanley George alimtaja mtu aliyekumbwa na mkasa huo kwa jina la Agustino Mtuti.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa tano asubuhi, baada ya kuibuka mapigano makali.
Stanley, alisema akiwa katika shughuli zake za uchomaji mkaa, alisikia kelele zikipigwa na watu ambao wanaomba msaada, baada ya wananchi kulalamikia kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mahindi .
Alisema baada ya hali hiyo, Mtitu alifika eneo la tukio na kuhoji sababu za wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.
“Baada ya kuhoji, mmoja wa wafugaji hao alitoka mbele yake na kumchoma mkuki mdomoni ambao ulitokea upande wa pili wa shingo,”alisema Stanley.
Alisema baada ya wafugaji kufanya tukio hilo na kubaini wanakijiji wamegundua, walikimbia na kuacha ng’ombe wao shambani ambao walichukuliwa na wananchi.
Alisema baada ya muda mfupi, wafugaji walirudi kwa lengo la kutaka kuwachukua ng’ombe wao ndipo mapigano makali yakazuka, huku wakulima wakijeruhiwa vibaya.
DIWANI
Diwani wa Kata ya Masanze, Bakari Killo (CCM), akizungumzia tukio hilo, alisema wafugaji walirudi mara ya pili na kufanya shambulio kubwa kwa lengo la kutaka kuteka mifugo yao.
Alisema katika harakati hizo Mwenyekiti wa Kijiji cha Dodoma, Stephano Daud, Mwenyekiti wa Kitongoji, George Andrea na mkazi wa eneo hilo, Saimo Luhoga walijeruhiwa vibaya.
Alisema baada ya kuona machafuko yametulia walifanya jitihada za kuwafikisha majeruhiwa wote Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jakob alisema majeruhi Mtitu alipokewa juzi saa 10 jioni na kupelekwa moja kwa moja chumba cha upasuaji ambako walifanikiwa kumtoa mkuki huo .
“Kutokana na timu ya madaktari wangu kufanya kazi nzuri dakika 80, hivi sasa wanaendelea kushona ulimi, kurudishia fizi na meno…kiujumla hali yake inaendelea vizuri,”alisema Dk. Jakob.
MBUNGE
Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema), amelaani vikali tukio hilo na kuiomba Serikali kufanya kazi ya ziada ili kupugunguza mapigano hayo.
Alisema lazima iweke miundombinu sahihi kwa kila kundi ili kuepuka mwingiliano na hata mapigano yanayoweza kuzuilika kati ya wakulima na wafugaji.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulurich Matei alisema hadi jana jeshi hilo limewatia mbaroni wafugaji watatu, huku likiendelea na msako wa kumtambua mmliki wa mifugo iliyosababisha mapigano hayo.
Juzi Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, alisema Taifa linakabiliwa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.
Alisema hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje kama njugu.
Mbali na hilo amesema pia Taifa limegubikwa na tatizo kubwa la rushwa inayosababisha baadhi ya wananchi kuonewa, kudhulumiwa na kukosa haki zao huku wengine wakilazimika kutumikia vifungo magerezani jambo ambalo ni hatari.
Askofu Dk. Shoo aliyasema hayo wakati akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi katika ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini , Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.
Alisema katika kipindi hiki ni vema Serikali ikawa makini na kujitahadharisha na tabia ya kuwamilikisha wawekezaji wa kigeni maeneo makubwa kwani suala hilo limekuwa likisababisha migogoro mikubwa na wananchi jambo ambalo alidai ni dalili kubwa ya kutokea machafuko nchini ikiwa ni pamoja na kuwagawa Watanzania.
“Tuwe makini katika umilikishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji wa mataifa mengine jambo hili likiendelea hivi katika siku za usoni litatuondolea amani yetu kabisa.
“Ardhi ni kitu muhimu sana tusigawe kama Karanga, nchi yetu imekuwa na ukarimu wa kumilikisha wageni ardhi ni tofauti sana na nchi nyingine na iwapo halitaangaliwa upya amani yetu tumeiweka rehani,” alisema askofu Dk. Shoo.
Kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro, iliilazimu Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuunda kamati maalumu ya wataalamu ili kuweza kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Timu hiyo ilikuwa ikiongozwa na na Dk. Steven Nindi, Mkurugenzi Mkuu mpya wa tume hiyo ambapo itashughulika na kuhakiki mipaka ya vijiji sita ambavyo vina migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji na kusababisha maafa wilayani humo.
Vijiji vilivyozungukiwa na timu hiyo ni Bonde la Mpunga la Mgongola ambavyo ni Hembeti, Dihombo, Mkindo Sindoni, Mkindo kwa Boma, Kambala na Kikundi.
Hata mapigano ya kila wakati yamekuwa yakiripotiwa na kubabisha mauaji na mifugo baina ya wakulima na wafugaji kila wakati.