23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

CHANJO YA NYOKA YAISHTUA SERIKALI

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

NA Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

SERIKALI imewaagiza waganga wakuu wa mikoa na viongozi wa hospitali zote  kuhakikisha wanaingiza chanjo ya nyoka katika mfumo wa dawa za dharura.

Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Afya, Nsachris Mwamwaja, ilisema agizo hilo linatakiwa kutekelezwa mara moja.

Taarifa hiyo, imewaagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri zote kupitia kwa uangalifu takwimu za wagonjwa waliong’atwa na nyoka kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

Aliwataka kuwasilisha takwimu hizo wizarani kabla ya Januari 31, mwakani.

“Kama tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu huleta madhara ya kiafya, tunafahamu  tatizo hili lipo zaidi maeneo ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.

“Dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo, ilisema bei ya kununulia dawa hizi ni kati ya Dola za Marekani 55 hadi 85 sawa na Sh 118,250 hadi 182,750 kwa chupa dogo (vial).

“Kichupa hiki hutumika kwa wagonjwa wanne, baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu,” ilisema taarifa hiyo.

Pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kila mwaka huagiza dawa hizo kwa ajili ya mahitaji ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni Sh  200,000 kwa chupa kimoja.

“Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa washirika  wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika,” iliongeza taarifa hiyo.

Aliongeza “Kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalumu au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa bima mbalimbali za afya.

“Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika. Hivyo tukipata takwimu sahihi zitatusaidia kujua mahitaji halisi ya dawa ya sumu ya nyoka nchini. Itasaidia kuboresha upangaji, uagizaji na upatikanaji wa dawa hizo nchini,” alisema.

Pia MSD  imetakiwa kuweka utaratibu wa haraka wa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei,” alisema.

Kutokana na hali hiyom  Watanzania wamehimizwa  kukata bima ya afya kwa sababu zinapunguza gharama.

“Wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) au Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya na mengine.

“Mfano gharama ya kujiunga na CHF katika halmashauri mbalimbali kwa kaya ni kati ya Sh 5,000  hadi  30,000 kwa mwaka…

“Kwa wagonjwa ambao watakuwa na bima ya afya, gharama za matibabu hayo zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa Bima,” alisema.

Wagonjwa ambao hawatakuwa na bima ya afya, watatakiwa kuchangia gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri itavyohitajika.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba kung’atwa na nyoka ni ajali na wananchi wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya nyoka ni mdogo,”ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles