Na DENNIS LUAMBANO- DAR ES SALAAM
MATUKIO mawili ya kigaidi yametokea Jumatatu ya wiki hii; moja limetokea katika Jiji la Berlin nchini Ujerumani ambako watu 12 wameuawa na wengine 50 wamejeruhiwa, baada ya mtu mmoja kuendesha lori na kwenda kuwagonga watu waliokuwa katika mkusanyiko wa Soko la Krismasi.
Hadi sasa vyombo vya usalama nchini humo vinaendelea kumtafuta mhusika wa tukio hilo, raia wa Tunisia ambaye hati zake za uhamiaji zilipatikana ndani ya lori hilo.
Taarifa zaidi zinasema raia huyo mwenye umri wa miaka 21, anayetafuta kibali cha uhamiaji anafahamika kwa maofisa wa usalama kwa makosa mengine.
Tukio la pili limetokea katika Jiji la Ankara, Uturuki, baada ya Balozi wa Urusi nchini humo, Andrey Karlov, kupigwa risasi tisa na Mevlut Altintas, ambaye ni ofisa wa zamani wa polisi wa nchi hiyo.
Taarifa zinasema Mevlut alimpiga risasi hizo Balozi Karlov wakati akihutubia katika maonyesho ya sanaa na yeye pia aliuawa papo hapo na maofisa usalama wa nchi hiyo. Wakati anatekeleza mauaji hayo alitamka maneno ya ‘Allah Akbar’, akimaanisha Mungu ni mkubwa, kisha akasema usisahau kuhusu Aleppo.
Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameapa kuyanyuka makundi ya kigaidi na kusema mauaji ya Balozi Karlov ni uchochezi wa kuharibu uhusiano kati ya mataifa hayo.
Mauaji ya Balozi Karlov yametokea siku kadhaa baada ya kutokea maandamano nchini humo ya kupinga ushiriki wa Urusi katika vita inayoendelea Syria, huku Urusi na Uturuki kwa sasa zikifanya kazi ya kuwahamisha raia kutoka Mji wa Aleppo.
Kwanini baadhi ya Waturuki waliandamana? Kimsingi, waliandamana kupinga makombora ya Urusi yanavyoendelea kuua watoto na raia wengine nchini Syria kwa kisingizio cha kuwaua magaidi wa Dola ya Kiislamu (IS), wanaotaka kuudhibiti mji huo.
Si hivyo tu, Urusi ndiyo mshirika mkubwa wa utawala wa Rais Bashar al-Assad na inamuunga mkono kwa kuanzisha operesheni kubwa za kijeshi nchini humo kwa kutumia manowari na vikosi vya majini kuzingira fukwe za nchi hiyo tangu vita hiyo ianze karibu miaka sita sasa.
Wakati Urusi ikifanya hivyo ili kuwadhibiti magaidi wa IS wanaotaka kuuangusha utawala wa Assad, lakini raia wasiokuwa na hatia wanaendelea kuuawa na kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao baada ya makazi yao kuharibiwa na makombora yanayotengenezwa ndani ya mapipa.
Kutokana na vitendo hivyo, ndiyo maana Mevlut akatekeleza mauaji ya Balozi Karlov, ikiwa ni kisasi cha matendo ya Urusi nchini Syria. Licha mauaji aliyoyafanya kuonekana ni ugaidi, lakini kwake ilikuwa ni namna nzuri ya kufikisha ujumbe kwa mtindo huo wa kulipiza kisasi kwa sababu wakati Urusi na dunia nzima ikilaani mauaji hayo, lakini inashindwa kulaani mauaji ya watoto na wanawake yanayotokea Aleppo. Unafiki uliopitiliza!
Wakati mauaji ya Ankara yakiwa ni kisasi, yale ya Berlin ni ugaidi. Tena ugaidi unaoanza kumea kwa kufanywa kwa mtindo mpya. Hata Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amenukuliwa akisema tukio hilo limemshangaza, limemtetemesha na kumhuzunisha na kuahidi wahusika wote watakamatwa na kushitakiwa.
“Ninayo imani kubwa kwa wachunguzi wa mkasa huu, pia naamini utasuluhishwa kwa kila hatua na wahusika wataadhibiwa vikali na sheria zetu,” anasema Merkel.
Kama nilivyosema kwamba mtindo wa ugaidi wa Berlin ni mpya na ulifanywa katika tukio kama hilo lililowahi kutokea Julai, mwaka huu katika mji wa Nice, Ufaransa, ambako watu 86 waliuawa baada ya lori kuwagonga wakiwa katika mkusanyiko.
Kimsingi, ugaidi huo unamaanisha kuwa, miji ya Ulaya iko mtanzikoni, kwa maana haiko salama tena, kwa sababu ni kawaida kwa matukio ya ugaidi kutokea katika msimu wa Krismasi.
Je, kwanini matukio ya ugaidi hayaishi? Je, ugaidi ni imani au kisasi?
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Oxford, neno ugaidi maana yake ni vitendo vya kutisha, mauaji na mashambulizi yanayofanywa ili kufikia malengo fulani fulani ya kisiasa.
Sasa kama hiyo ndiyo tafsiri ya ugaidi, je, magaidi wa Berlin wana malengo gani ya kisiasa? Maswali hayo yananitatiza, hasa ukilinganisha na matukio mengine ya kigaidi yaliyotokea siku za nyuma katika maeneo mbalimbali duniani.
Kama ni aina mpya ya ugaidi kwa maana mbinu zinabadilika au tukifuata tafsiri ya neno ugaidi kwa mujibu wa kamusi niliyoitaja hapo juu, je, kitendo cha majeshi washirika yakiongozwa na Marekani kuivamia Irak mwaka 2001 na kuanza kuupiga utawala wa Saddam Hussein waliyemnyonga Desemba, 2006 ni ugaidi au si ugaidi? Pia kitendo cha majeshi hayo hayo cha kuivamia Libya kisha Oktoba, 2011 wakamuua mtawala wake, Kanali Muammar Gaddafi ni ugaidi au si ugaidi?
Kwa sababu waliwaua viongozi hao kwa visingizio vya kipuuzi ambavyo hadi leo havijathibitishwa, mathalani Saddam walisema ana silaha za maangamizi ya halaiki na Gaddafi walisema ni dikteta anayeminya demokrasia nchini mwake.
Pia waliharibu mali na miundombinu, huku kampuni za nchi washirika zikizawadiwa kandarasi za kuzijenga upya kwa malipo ya kunyonya malighafi ya mafuta yanayopatikana kwa wingi katika nchi hizo.
Hiyo ni mifano michache kati ya mingi ambayo baadhi ya wachambuzi huru wa kitaifa na kimataifa wamewahi kuhoji, pia na mimi nimehoji kwa kukazia hoja yangu kama ugaidi ni zaidi ya imani?
Pengine matukio ya kigaidi yameongezeka zaidi baada ya Marekani kutangaza rasmi kuwa vita hiyo ni ya dunia nzima, ndiyo maana suala la imani linaingia.
Lakini nihitimishe kisa mkasa hiki kwa kupinga kisasi cha mauaji kilichofanywa na Mevlut, pia napinga raia wasiokuwa na hatia wanavyoendelea kuuliwa na wengine kupata vilema vya kudumu nchini Syria, baada ya kupigwa makombora ya ndege zisizokuwa na rubani, kwa sababu matukio hayo ndiyo yanazaa imani hiyo na ndiyo maana ni ndoto za mchana kuyamaliza kwa kuwa imani hiyo itaendelea kupandikizwa kizazi hadi kizazi. Kwa sababu baadhi ya jamii fulani fulani za watu zinaamini zinaonewa na kawaida kwa binadamu akidhani anaonewa anashikilia zaidi imani yake. Kwa hiyo hata Mevlet na baadhi ya vijana wanaojiunga IS wanashikilia zaidi dini yao kwa vile ndiyo sehemu pekee inayowapa matumaini kwa kuwa wanaamini wanafanyiwa dhuluma na baadhi ya tawala mbalimbali hapa duniani na ndiyo maana wanalipiza kisasi.