29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA YAWAPA MASHABIKI ZAWADI YA KRISMASI

5

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Simba imewapa mashabiki wake raha ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, baada ya kuifunga timu ya JKT Ruvu bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

 Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi, Hans Mbena kutoka Tanga, ilikuwa na upinzani wa aina yake huku kila timu ikitafuta ushindi.

Dakika mbili baadaye Simba walianza kuliandama lango la JKT Ruvu baada ya mshambuliaji, Pastory Athanas, kuwatoka mabeki wa maafande hao, lakini akaangushwa chini na beki Hassan Dilunga na kuwa faulo ambayo ilipigwa na Abdi Banda na kudakwa na kipa wa JKT Ruvu, Hamisi Seif.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku kila timu ikihitaji kupata bao ambapo dakika ya 15 mchezaji wa JKT Ruvu, Edward Joseph, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu, Athanas.

Simba walikosa bao katika dakika ya 17 baada ya Athanas kupiga shuti hafifu lililodakwa na kipa wa JKT Ruvu, Seif.

Katika dakika ya 20 mchezaji wa Simba, James Kotei, alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumkwatua mchezaji wa JKT Ruvu, Dilunga.

Simba walikosa bao katika dakika ya 29 ambapo Banda alipiga mpira wa kichwa na kutoka nje baada ya kona iliyopigwa na Mohamed Hussein huku Shiza Kichuya akikosa bao katika dakika ya 33 baada ya kupiga mpira mrefu uliotoka nje.

Dakika ya 45 kabla ya kwenda mapumziko, Simba walipata bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Muzamiru Yassin, baada ya kupokea krosi iliyopigwa na Kichuya, huku akiwa chini baada ya kudondoka wakati alipokwenda kuokoa mpira, hivyo Wekundu hao wa Msimbazi kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao hilo moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko kwa kumtoa Juvier Bukungu na kuingia Hamad Juma huku JKT Ruvu nao wakifanya mabadiliko katika dakika ya 51 kwa kumtoa Ally Bilal na nafasi yake kuchukuliwa na Najim Magulu.

JKT Ruvu walijitahidi kutafuta bao la kusawazisha na kujikuta wakishambuliwa na katika dakika ya 57, Kichuya alikosa bao baada ya kupiga shuti lililogonga mwamba na kurudi uwanjani na mabeki wa JKT Ruvu kuokoa.

JKT Ruvu walifanya mabadiliko katika dakika ya 59 kwa kumtoa Salim Gilla na nafasi yake kuchukuliwa na Atupele Green, huku dakika ya 61, Michael Aidan, akionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu, Mohamed Hussein.

Simba nao walifanya mabadiliko katika dakika ya 62 kwa kumtoa Mohamed Ibrahim na kuingia Jamal Mnyate, ambapo katika dakika ya 65, Kichuya alikosa bao baada ya kupiga shuti lililotoka nje akipokea pasi ya Athanas.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana huku katika dakika ya 80, Simba walifanya tena mabadiliko kwa kumtoa James Kotei na kuingia Said Ndemla na hadi dakika 90 zinamalizika, Simba walitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0.

Kwa matokeo hayo Simba wanafikisha pointi 41 wakiwaacha watani wao Yanga walio nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 37.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Mtibwa Sugar wameifunga Ndanda FC mabao 2-0 katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, huku Azam FC ikiwa ugenini mjini Songea mkoani Ruvuma ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Majimaji ya Songea.

Kagera Sugar wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Kaitaba, wameifunga Stand United bao 1-0 huku Mwadui  wakiifunga Mbao FC bao 1-0 wakati Mbeya City wakitoka suluhu na Toto Africans.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles