25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AKAGUA ENEO LA UJENZI WA NYUMBA ZA MAGEREZA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametembelea Gereza la Ukonga na kukagua eneo la ujenzi wa makazi ya askari wa magereza unaotarajiwa kuanza baada ya wiki tatu zijazo.

Akizungumza Dar es Salaam jana na askari magereza kabla ya kufanya ukaguzi huo, Majaliwa alisema ziara aliyoifanya ni ufuatiliaji wa maagizo ya Rais Dk. John Magufuli aliyoyatoa wakati alipoenda kukagua gereza hilo.

Novemba 29, mwaka huu, Rais Magufuli alifanya ziara gerezani hapo na kupokea taarifa ya uhaba wa nyumba za kuishi askari wa jeshi hilo zipatazo 9,500 na akaagiza zitafutwe Sh bilioni 10 haraka ili kupunguza tatizo hilo.

Kuhusu ujenzi huo, Majaliwa alisema amefarijika kukuta Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wako eneo la kazi na wameanza kusafisha eneo hilo.

“Nimefarijika kukuta TBA wako kazini na nimeelezwa hatua inayofuata ni upimaji wa sampuli za udongo kabla hawajaanza kujenga msingi. Nawapongeza TBA kwa kazi nzuri wanazofanya za ujenzi wa nyumba zenye viwango na kwa haraka, kama tulivyoona kule Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nyumba za Magomeni Kota,” alisema.

Alisema Serikali inatambua mchango uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne katika suala la makazi ya askari kama vile wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.

“Nia ya Serikali ni kuhakikisha makamanda wote wanapata nyumba nzuri ili waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa, wakiwa na uhakika familia zao zimetulia katika makazi bora,” alisema Majaliwa.

Alisema katika ziara alizozifanya katika mikoa mbalimbali, alitembelea magereza ya Isanga, Msalato (Dodoma), Lindi, Singida na Keko (Dar es Salaam) na alikuta nyumba za askari hazina ubora na kama zipo zimechakaa sana.

Awali, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa nyumba hizo, Kaimu Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk. Juma Malewa, alisema wanamshukuru Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa makazi ya askari na wao watafanya kazi zote zisizo za kitaalamu ili kuokoa fedha za Serikali na badala ya kulipwa watu binafsi, fedha hizo zitatumika kuongeza nyumba zaidi.

“Tumekubaliana na TBA, kazi zote zisizohitaji utalaamu kama kufyatua matofali, kubeba mizigo au kufyeka zitafanywa na askari wetu pamoja na wafungwa ili tuokoe gharama zote hizo, na badala ya kulipa watu binafsi, fedha hizo zitumike kujenga nyumba nyingine 80,” alisema Dk. Malewa.

Alisema wamejipanga kufanya kazi hizo kwa saa 24 kila siku ili kuokoa muda ambao TBA walikuwa wameuweka wa kukamilisha ujenzi kwa miezi minane.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TBA, Baltazar Kimangano, alisema wanatarajia kuanza ujenzi ndani ya wiki tatu baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi wa sampuli za udongo kutoka Taasisi ya Bico ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema wanatarajia kujenga majengo manne ya ghorofa sita kila moja ambayo kwa ujumla yatakuwa na nyumba 240 zenye ukubwa wa vyumba viwili vya kulala kila moja.

Pia watajenga majengo mengine mawili ya ghorofa sita yatakayokuwa na nyumba 80 zenye ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala kila moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles