24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI RORYA LAWAMANI

Mbunge wa Rorya, Lameck Airo (CCM)
Mbunge wa Rorya, Lameck Airo (CCM)

Na Peter Fabian – RORYA

ASKARI Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, wameingia matatani baada ya kudaiwa kuwanyanyasa wananchi wa kata za Jimbo la Rorya, Mkoa wa Mara wanapokwenda katika magulio na minada ya mifugo.

Habari zinadai kuwa baadhi ya polisi huwavizia wananchi maeneo ya porini na kuwakamata na kuwashikilia hadi wanapotoa fedha ndipo huwaachia.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumapili kwa nyakati tofaiti katika maeneo ya kata za Shirati, Utegi, Labwoli, Kumuge, Kisumwa na Nyamuga wakiomba kuhifadhiwa majina yao kwa kuhofia kukamatwa na polisi hao, wamelalamikia kuwapo kero hiyo na unyanyasaji unaofanywa na askari hao, hasa siku za magulio na minada ya Nyamaguku, Shirati, Mtana na Randa.

“Siku ya gulio na mnada wa mifugo katika maeneo ya Nyamaguku, Shirati, Mtana na Randa, askari polisi huja kwa wingi wakiwa na silaha kwenye pikipiki (bodaboda) sita wakiwa wamebebana wanazokuwa wamezikamata kwa wananchi na wengine kwenye magari ya Polisi PT 1691 ya Kanda Maalumu Tarime na Rorya na ya OCD Utegi,” alieleza mmoja wa wananchi.

Mwananchi mwingine alidai kuwa askari hao wamekuwa wakivizia siku za magulio, minada na masoko ambapo wamekuwa na tabia ya kuwaamsha kuanzia saa 10 alfajiri wakidai wanasaka nyavu haramu na samaki wachanga na wakikosa huwavizia waendesha badaboda na kuwafukuza kwa gari na pikipiki hadi wawapatie fedha.

“Hii ni kero kubwa kwa vijana waendesha bodaboda na wananchi wanaotumia usafiri huo. Umeonekana kuwa ni mradi wa askari polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya, ambao wamekuwa wakiwakamata na kuwaomba fedha na wanapokosa huwaomba hadi kuku na hata wanapodai stakabadhi (risti) huambiwa kwa kufokewa huku wakitishiwa pikipiki zao kupandishwa kwenye magari,” alisema mmoja wa waendesha bodaboda.

Mbunge wa Rorya, Lameck Airo (CCM), alikiri kuwa amekuwa akipata malalamiko ya wananchi na viongozi wa vijiji na kata juu ya kuwapo kwa askari wanaowanyanyasa na kuwakamata waendesha bodaboda kwa kuwavizia maeneo ya porini kisha kuwatoza fedha hadi kuwaomba kuku na mbuzi bila kuwaeleza makosa yao.

“Nimekuwa nikikutana na wakuu wa polisi kila mara na hata kumweleza Kamanda wa Kanda Maalumu ya Tarime na Rorya (RPC), Andrew Sata, lakini hali hiyo husitishwa kwa muda na kisha huibuka tena kwa nguvu kubwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles