Na FARAJA MASINSDE,
KILA mtu anatamani kusoma nje ya nchi hususan Ulaya ambako baadhi ya watu wamekuwa wakiamini kuwa kusoma au kupata ujuzi kwenye vyuo hivyo vya ng’ambo kutawawezesha kupata fursa zaidi za ajira ikilinganishwa na kusoma kwenye vyuo vya ndani.
Kumekuwapo baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwapata wanafunzi wa kigeni pindi wanapokuwa ng’ambo.
Hii inatokana kwamba nchi nyingi zimekuwa haziweki mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kigeni, hata inapotokea wamekumbwa na misukosuko serikali za nchi hiyo zimekuwa zikichelewa kuchukua uamuzi au kuwatetea wanafunzi hao.
Hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya wanafunzi na wazazi  kuwa na hofu ya kwenda kusoma nje ya nchi zao.
Matukio kadhaa yasiyo ya kufurahisha yamewakumba wanafunzi wa kigeni, hali hiyo imekuwa ikitafasriwa kama ni kawaida kwa mataifa yaliyo na vyuo bora nje ya nchi jambo ambalo si kweli.
Kama ndoto zako au hata za mtoto wako ni kusoma na kupata ujuzi nje ya nchi kwenye vyuo vilivyoendelea na kujenga wasifu wake vizuri utakaomsaidia kupata kazi kirahisi ndani na nje ya nchi na bado hujajua ni nchi gani ambayo mwanao atasoma akiwa salama na kukarimiwa vizuri, makala hii itakupa mwanga.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Ulaya EU miezi michache iliyopita, imeorodhesha nchi nane zinazoongoza kwenye kuwakarimu wanafunzi wa kigeni.
 Uingereza
Nchi hii imepata asilimia 0.7 ya kukarimu wageni huku ikinyakua asilimia 0.5 ya wanafunzi wanaohitimu kwenye vyuo vyake.
Licha ya kwamba nchi hii iliibuka kinara kwa kuwa na wanafunzi wengi wa kigeni kati ya nchi 35 za bara hilo lakini ilikuwa na asilimia 40 ya wanafunzi wake ambao walihitimu nje ya vyuo vya nchi hiyo kwa mwaka 2012-2013 jambo ambalo lilifanya ipunguziwe alama kwenye ripoti hiyo.
Mbali na ‘doa’ hilo, ni wazi kuwa Uingereza imekuwa ikisifika kwa kuwa na mazingira mazuri kwa wanafunzi wa kigeni ikiwamo kuwapa msaada wa karibu na kuwashirikisha kwenye fursa mbalimbali za kiuchumi.
 Ubiligiji
Ina asilimia 2.4 ya ukarimu kwa wanafunzi huku kiwango cha wanafunzi wanaohitimu masomo yao nchini humo kikiwa ni asilimia 3.3 ambapo pia imekuwa ikisifika kwa kuwahamasisha wananchi wake juu ya watoto wao kujifunza lugha za kigeni walau 15 kwa mwaka.
Nchi hii haijapishana na Uingereza katika kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi sanjari na kuwawezesha kiuchumi ambapo katika kulitekeleza hilo imekuwa na mikakati mbalimbali ukiwamo ule wa ‘Flemish community’  wenye lengo la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 inakuwa na asilimia 33 ya wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali wanaokwenda kusoma nchini humo.
Kwasasa asilimia 48 ya wanafunzi wa kigeni wanaosoma nchini humo ni kutoka Ufaransa.
 Denmark
Hii ina asilimia 1.3 ya ukarimu kwa wanafunzi huku ikiwa na asilimia 1.7 ya wanafunzi wa kigeni wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini humo.
Denmark ni miongoni mwa nchi chache za Ulaya zinazotoa msaada mkubwa zaidi kwa wanafunzi wa kigeni karibu wote wanaofika kuchukua masomo yao nchini humo, pia inatoa ushirikiano zikiwamo taarifa mbalimbali kwa wanafunzi.
Pamoja na mambo mengine imeweka mkazo wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anajifunza lugha mbili kwa wakati mmoja kwa kipindi cha walau miaka mitano huku akipata mkopo na msaada mkubwa kutoka serikalini.
Nchi nyingine ambazo zimekuwa na alama za juu zaidi ni pamoja na Ujerumani ambayo ina asilimia 3.9 ya kukarimu wanafunzi wa kigeni huku ikiwa na asilimia 54.1 ya wanafunzi wa kigeni wanaohitimu masomo yao nchini humo.
Lakini pia imekuwa ikitoa misaada ya hali na mali kwa wanafunzi wote wa kigeni wanaofika nchini humo. Nyingine ni Bulgaria yenye ukarimu wa asilimia 7.8 kwa wanafunzi wa kigeni na asilimi 6.6 ya wanaohitimu. Asilimi 52 ya wanafunzi wake wanatoka nchini Uturuki.
Nyingine ni Uholanzi, Luxembourg na Slovakiam. Chaguo ni lako mwanafunzi na mazazi kumpeleka mwanao nje au la kwani nchi hizo zote zina mazingira rafiki ya taaluma na hali ya juu.