KINSHASA, DRC
WAANDAMANAJI 26 wameuawa na wengine kadhaa kukamatwa katika maandamano ya kupinga Rais Joseph Kabila kuendelea kubakia madarakani hata baada ya muda wake kumalizika kikatiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) juzi.
Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch, limesema wanajeshi na maofisa wa polisi walirusha risasi ovyo kwa waandamanaji, jambo linalozusha wasiwasi kuwa huenda watu wengi zaidi wameuawa katika siku ya kwanza baada ya muda wa Rais Kabila kumalizika.
Mtafiti wa shirika hilo, Ida Sawyer, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba mauaji ya siku ya Jumanne yalifanyika katika mji mkuu, Kinshasa, mji wa kusini wa Lubumbashi na maeneo mengine.
Mashuhuda walisema kikosi maalumu cha rais, Republican Guard, kilikuwa kikipita nyumba kwa nyumba kuwasaka na kuwakamata vijana.
Mjini Kinshasa, waandamanaji waliyachoma moto makao makuu ya chama tawala.
Katika Kitongoji cha Matonge, watu walijitokeza kucheza mpira barabarani kuzuia magari kupita kama aina moja ya kuandamana, huku kukiwa na kiwango kikubwa cha wanajeshi na polisi mitaani.
“Kabila ameisaliti nchi yetu. Lazima aondoke,” alisema Jean-Marcel Tshikuku, fundi gereji.
“Alitangaza serikali mpya mwisho wa muhula wake. Ni matusi. Hatumtaki tena. Hatutaki mazungumzo. Tunataka aende. Aondoke tu.”
Kwa mujibu wa Katiba ya Kongo, muda wa Rais Kabila kubakia madarakani ulimalizika Jumatatu iliyopita na haruhusiwi kuwania muhula mwingine.
Mazungumzo ya kusaka mwafaka wa kisiasa kati ya chama tawala na upinzani yalikwama mwishoni mwa wiki na kutazamiwa kurejea tena jana, chini ya upatanishi wa Kanisa Katoliki.
Baada ya machafuko ya juzi, hali ya utulivu iliripotiwa jana wakati Kanisa Katoliki likiwakutanisha viongozi wa upinzani na Serikali.