Na ELIUD NGONDO, CHUNYA
ZAIDI ya Sh milioni 85 zinahitajika katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya, mkoani Mbeya kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitalini hapo.
Akizungumza jana kwenye harambee ya uchangiaji wa vifaa vya ujenzi wa chumba hicho na fedha, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya hiyo, Stanford Mwakataghe, alisema wananchi na wadau wanatakiwa kuchangia ujenzi huo.
“Wilaya yetu kwa sasa ina miaka 74 tangu ianzishwe na mwakani kuna mkakati wa kusherehekea miaka 75.
“Pamoja na mikakati hiyo, hakuna chumba cha kuifadhia maiti katika hospitali ya wilaya, hali ambayo imekuwa ni shida kwa wananchi.
“Kutokana na tatizo hilo, kumekuwa na ulazima wa kuzika watu haraka kwa sababu hakuna sehemu ya kuhifadhi miili kwani hata chumba kilichopo kwa ajili ya maiti, kina uwezo wa kuhifadhi mwili mmoja.
“Kutokana na tatizo hilo, wananchi wamekuwa wakipata shida kwani hata sisi watumishi inatuwia vigumu kutunza miili ya wapendwa wetu kwa sababu hakuna sehemu ya kuhifadhia,” alisema Mwakataghe.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Sostenes Mayoka, alisema ujenzi wa chumba hicho unategemea sana wadau mbalimbali wa wilaya hiyo pamoja na mchango wa halmashauri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Sophia Kumbuli, alisema fedha zilizopatikana wakati wa harambee hiyo, zitaelekezwa katika ujenzi wa chumba hicho cha maiti.