HERIETH FAUSTINE NA JULIETH JULIUS(DSJ)-DAR ES SALAAM
IDARA ya Uhamiaji imekamata mtandao wa kutengeneza vibali, mihuri na hati za kughushi kwa wageni wanaoingia nchini kinyume cha sheria.
Mtandao huo umekamatwa baada ya kufanyika kwa operesheni iliyofanywa na maofisa wa idara hiyo ambapo waligundua kuwepo kwa wageni walioingia nchini kinyume cha sheria na kufanya kazi bila vibali pamoja na madanguro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa, John Msumule, alisema pia katika msako huo waliweza kubaini mtandao unaohusika na utengezaji wa vibali feki pamoja na wageni wa kutoka nchi za nje kinyume cha sheria.
Msumule alimtaja mtuhumiwa Mohammed Magamba kuwa alikutwa na hati nne za nchi mbalimbali zikiwa tayari zimegongwa mihuri feki.
“Mohammed Magamba amekuwa akishirikiana na mtandao wake na wamekuwa wakifanyakazi ya kuchukua hati za wageni na kuwagongea mihuri feki, kuwatengenezea vibali vya kughushi kwa wageni ili waweze kufanikisha mambo mbalimbali.
“Pia amekutwa na hati nne za kutoka nchi ya Nigeria, Somalia, Uingereza na Botswana zikiwa tayari zimeshagongewa mihuri tayari kwa ajili ya shughuli mbalimbali,”alisema Msumule.
Alisema kupitia hati hizo, idara hiyo itawatafuta wenye hati hizo ili kuweza kufahamu walikuwa wakitaka kuzitumia kwa mambo gani.
Aidha Msumule alisema katika tukio lingine, idara hiyo imekamata watu wawili, mmoja raia wa India na mwingine mtanzania ambao walikuwa wakishirikiana kuwaingiza wasichana nchini kwa ajili ya biashara ya ukahaba.
Alisema watu hao wamekuwa wakichukua wasichana kutoka Nepal na India na kuwaingiza katika madanguro kwa ajili ya kufanya biashara ya ukahaba ambayo imekuwa ikipigwa marufuku nchini.