33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

NEC YA CCM KUFANYIKA LEO DAR

15

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

KIKAO cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), leo inatarajiwa kukutana Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. John Magufuli.

Kikao hicho kimetanguliwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho (CC), kilichofanyika jana ambacho pamoja na mambo mengine, kimefanya tathimni ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, na kuibuka na mambo kadhaa ambayo yatafikishwa mbele ya wajumbe wa NEC.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, alisema tathmini hiyo ya uchaguzi, iliyofanywa na CC ni sehemuya utamaduni wa CCM kila baada ya Uchaguzi Mkuu.

“Tathmini hizi hutusaidia sana, kujua wapi tulifanya vizuri na wapi hatukufanya vizuri na mengineyo yote yaliyokuwa sehemu ya ushiriki wa chama katika Uchaguzi Mkuu, na tumekuwa tukifanya hivi katika chaguzi zote hali ambayo imeifanya CCM kuimarika zaidi,” alisema Nape.

Alisema mapendekezo au hoja zote zilizoibuliwa na wajumbe katika kikao hicho cha Kamati Kuu, zitawasilishwa katika kikao cha NEC.

Nape alisema kutokana na kufanyika vizuri na kwa umahiri mkubwa, Kikao cha Kamati Kuu kilimalizika jana. Awali kilipangwa kufanyika kwa siku mbili.

Katika kikao hicho cha NEC, inatarajiwa Dk. Magufuli huenda akafanya mabadiliko ya sekreterieti ya chama baada ya kufanya uteuzi kwa baadhi ya wajumbe wake ambao amewapa nafasi ndani ya Serikali.

Walioteuliwa hivi karibuni kuwa mabalozi ni Dk. Emmanuel Nchimbi, Dk. Pindi Chana ambao wote ni wajumbe wa Kamati Kuu na Naibu Katibu Mkuu Bara, Rajab Luhwavi.

Dk. Magufuli pia huenda akaamua hatima ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitaka kupumzika siasa na kubaki mwanachama wa kawaida.

Julai 23, mwaka huu baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Dk. Magufuli alimteua tena Kinana kuendelea na nafasi yake ya Katibu Mkuu wa chama hicho, ingawa yeye aliomba kujiuzulu.

Akihutubia Mkutano Mkuu wa chama hicho kwa mara ya kwanza, Dk. Magufuli alieleza kupokea barua ya kujiuzulu kwa Kinana muda huohuo akiwa katika mkutano huo na kuisoma kabla ya kuhitimisha hotuba yake.

Katika barua hiyo, Kinana alieleza sababu ya kutaka kujiuzulu kuwa ni kutimiza matakwa ya utaratibu na utamaduni wa CCM wa kuachiana madaraka.

Baada ya kusoma barua hiyo, Dk. Magufuli alitangaza kumteua tena Kinana na sekretarieti yake yote hadi hapo atakapotangaza tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles