Dk. Fredirick Mashili, MD, PhD
KUPUNGUZA mafuta na uzito wa mwili ni mojawapo ya faida za kiafya za mazoezi. Mafuta na uzito vikizidi mwilini huchangia kusababisha magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya moyo, baadhi ya saratani na maumivu sugu ya viungo.
Hata hivyo, ili mazoezi yaweze kufanya kazi hiyo ya kupunguza mafuta na uzito, kuna mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa kabla, wakati na hata baada ya kufanya mazoezi hayo. Pia kuna vitu vingine kama aina na muda wa kufanya mazoezi, ambavyo pia ni muhimu kuvizingatia.
Haya hapa mambo matatu unayotakiwa kuzingatia ili mazoezi unayofanya yaweze kukusaidia kupunguza uzito.
- Aina ya mazoezi
Katika makala zilizopita tulizungumzia aina kuu tatu za mazoezi, aerobics (cardio), mazoezi ya kusukuma au kunyanyua uzito (Resistance) na mazoezi ya kulainisha na kunyoosha viungo (flexibility exercise).
Katika aina hizi tatu za mazoezi, mazoezi ya aerobics ndiyo huufanya mwili kutumia mafuta kwa wingi hivyo kusaidia katika kupunguza mafuta na uzito. Lakini ikumbukwe pia kwamba mazoezi ya kuvuta au kusukuma uzito (resistance exercise) ni muhimu pia katika kuendeleza matumizi ya mafuta baada ya kusita kufanya mazoezi. Kwa kifupi, mazoezi ya aerobics huuwezesha mwili kuchoma mafuta wakati ukifanya mazoezi, na yale ya resistance huufanya mwili kuendelea kuchoma mafuta hata baada ya kuacha kufanya mazoezi.
Ili kupunguza mafuta na uzito wa mwili, ni muhimu kufanya mazoezi ya aerobics kwa wingi na kuchanganya na mazoezi ya resistance angalau mara mbili kwa wiki.
- Kiasi, aina na muda wa chakula
Kuna watu ambao ni hodari sana katika kufanya mazoezi, lakini ni hodari pia katika kula. Kwa kufanya hivyo hujikuta hawapungui licha ya kufanya mazoezi. Ikumbukwe kwamba kupunguza mafuta mwilini huchangiwa kwa asilimia 70 na aina, kiasi na muda unaokula milo yako. Mazoezi huchangia asilimia 30 tu. Kwa maana hiyo unapofanya mazoezi huna sababu ya kwenda kula chakula kingi au kuzidisha kiasi cha wanga na mafuta mabaya katika mlo wako. Licha ya kwamba mazoezi hukuongezea hamu ya kula, fahamu kwamba kupungua hutokana na kuingiza nguvu joto (calories) kidogo zaidi ya zile unazotumia. Nguvu joto huingia mwilini kwa kupitia vyakula tunavyokula na hutoka mwilini kwa kufanya mazoezi. Kwa maana hiyo unatakiwa udumishe uwiano mzuri kati ya kiasi cha mazoezi na chakula unachokula.
- Muda wa mazoezi
Unaweza ukawa na mahudhurio mazuri katika mazoezi, lakini kama hutimizi muda unaotakiwa unaweza usinufaike na faida za mazoezi. Ifahamike kwamba mwili wako huanza kutumia mafuta katika dakika ya saba mpaka ya 15 mara baada ya wewe kuanza kufanya mazoezi kama kukimbia (jogging). Kwa maana hiyo ni muhimu kufanya mazoezi kwa muda usiopungua dakika 20 ili kuweza kuchoma angalau kiasi kidogo cha mafuta. Lakini pia ni muhimu kutimiza angalau dakika 10 katika zoezi la aina moja kabla ya kuhamia katika zoezi lingine. Unapohamia katika zoezi lingine kabla ya kutimiza dakika 10 unakuwa umekatisha muda hivyo kutokufikia wakati ambao mwili huanza kutumia mafuta.
Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS).   0752255949 [email protected]  www.jamiihealthtz.com  www.jamiiactive.org