24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO YANAYOSABABISHA MATATIZO WAKATI WA KUJIFUNGUA – 2

150824151028-pregnant-woman-exlarge-169

Na DK. JOACHIM MABULA

WIKI iliyopita tulianza kuangalia mambo mbalimbali yanayosababisha matatizo wakati wa kujifungua kama vile kutojitunza vizuri kwa mwanamke kipindi cha ujauzito, kukosa matibabu yanayofaa na kukosa huduma nzuri za afya kipindi cha ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

Leo tutaendelea kuangalia mambo mengine na mchango wa wahudumu wa afya katika uzazi salama.

 Je, kupata huduma nzuri za afya kunamaanisha kwenda kliniki kila juma? La, si lazima. Kuhusu matatizo ya kawaida yanayowapata wanawake wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), liligundua kwamba wanawake walioenda kliniki mara nne tu wakati wa ujauzito walipata matokeo yale yale kama wanawake walioenda kliniki mara 12 au zaidi.

Umbali wa huduma za afya

Watanzania wengi wanapatikana maeneo ya vijijini ambako huduma za afya hazipo za kutosha hivyo kulazimisha wajawazito kusafiri umbali mrefu kusaka huduma bora za afya. Katika baadhi ya maeneo usafiri ni wa taabu na wa gharama kitu kinachochangia wajawazito kushindwa kumudu.

Asilimia 47 tu ya wajawazito hujifungua kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, asilimia 46 wanaozaa huhudumiwa na kusaidiwa na wataalamu wa huduma za afya. Kati ya asilimia 53 ya wanaozalia nyumbani, asilimia 31 husaidiwa na ndugu zao, asilimia 19 husaidiwa na wakunga wa jadi na asilimia 3 hujifungua bila msaada wowote.

Kutokuwa na uwezo wa kugharimia huduma za afya

WHO linasema vifo vya wajawazito maeneo ya vijijini vipo juu hasa kwenye jamii masikini. Wanawake wenye vipato vya juu wanatarajia kujifungua kwa msaada wa wataalamu wa afya kwa asilimia 87 ikilinganishwa na wanawake wenye vipato duni ambayo ni asilimia 13 tu.

Kutokuwa na elimu

Wajawazito wengi wanaopata matatizo ni wale ambao hawakusoma au hawana taarifa kuhusu afya ya uzazi pamoja na uzazi salama.

Mila potofu

Jamii nyingi za vijijini bado wana mila potofu zinazoendekeza kujifungulia nyumbani ambapo huamini anayejifungulia nyumbani ndio shujaa kitu ambacho kinaweza kusababisha matatizo kwa kuwa hatopata huduma stahiki.

Mchango wa wahudumu wa afya katika uzazi salama

Wao huchunguza rekodi za matibabu za mama na kufanya uchunguzi ili kuona kama kunaweza kuwa na hatari na hivyo kuzuia matatizo yanayoweza kumpata mama na mtoto wake. Wakati hatari zaidi kwa mjamzito ni pindi anapopatwa na maumivu ya kuzaa hadi anapojifungua. Wanapotambua hatari zinazohusiana na mjamzito huchukua hatua zinazofaa au kumsaidia mjamzito kuchukua hatua hizo, wanachangia afya nzuri kwa mama na mtoto wake ambaye bado hajazaliwa.

Wanaweza kupima damu na mkojo ili kuchunguza upungufu wa damu, maambukizo, ikiwa damu ya mama na mtoto hazipatani na magonjwa. Magonjwa hayo yanaweza kuchangia kisukari, surua ya rubella, magonjwa ya zinaa na ugonjwa wa figo, ambayo yanaweza kufanya shinikizo la damu lipande.

Itaendelea wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles