NA CHARLES KAYOKA,
MHESHIMIWA Rais Magufuli, kwa sababu hivi karibuni ulizungumzia nia yako ya kukuza utalii. Ukasema kuwa ungependa nchi iwe na ndege inayoweza kubeba kutoka nchi wanakoishi na kuwa ungependa kuona tunashirikiana na nchi kama Morocco katika masuala ya utalii na hasa kwa kutusaidia kutuletea watalii, nimeona nitoe dukuduku langu kuhusiana na hilo! Nadhani utapata nafasi ya kusoma, japo unayo mengi ya kusoma!
Kwanza nafahamu kuwa sekta ya utalii inatoa mchango mkubwa wa pato la Taifa. Asilimia 17 na ushee sio jambo dogo. Lakini nafahamu pia kuwa nchi ilijiwekea mpango mkuu wa kuendeleza sekta ya utalii (National Tourism Master plan) Mpango uliolenga kufanya maboresho mkakati kwa kila aina ya kivutio. Na mpango huu sijauona ukifanya kazi kwa kiwango kile cha ahadi ilichotoa. Sababu kubwa ni fedha!
Fedha zinahitajika kwanza kwa ajili ya kuutangaza utalii wenyewe! Utalii unahusu kuona, sio kusikia wala kusoma..Mtalii anapokuwa huko aliko anataka kuona kivutio unachomwitia kikoje, kwa macho! Na mtalii huyu anapelekewa taarifa kutoka sehemu mbalimbali wakimwalika aende akatembelee. Hili linahitaji uwekezaji na uwekezaji ambao hautakiwi kusimamishwa, ni gharama na gharama sana kama kweli tunataka kuufanya utalii ujulikane nchini na nje.
Unaangalia kwa mfano, tunataka kuwa na utalii wa ndani uimarishwe, ninaunga mkono, lakini ni kweli tumevitangaza vivutio hadi watu wakapata hamasa? Hatujaweza… tunaambiwa tu nendeni mkatembelee Mikumi, lakini hatujengewi kwa kuonyeshwa hamasa nini tutaenda kuona.
Ukiishi Dar es Salaam unaweza kudhani hakuna utalii na hatuzungukwi na vivutio vya utalii. Ukisafiri kwenye ndege za Tanzania hakuna chochote kinachohusu utalii, vivyo hivyo ukisafiri kwenye mabasi na meli. Ukikaa kwenye baa tunakunywa soda au bia, ni mpira, ni filamu za nje au Bongo Movie. Na kwenye ndege tunasafiri kimya kimya. Majarida hamna. Kuna ndege kama Emirates na KLM zinazokuja Tanzania niambie tumeweka nini kuwavutia watalii. Utangazaji unahitaji fedha na uwekezaji, tukijua kuwa fedha hizo zitarudi tu kwa kuwavuta watalii wengi.
Na nadhani watendaji wetu katika idara na mamlaka zinazohusu utalii wamepwelea katika mbinu na mikakati ya kuutangaza utalii wetu. Kwanza mitaala ya mafunzo ya utalii na usimamizi wa hoteli hauhusishi mafunzo ya utangazaji na usimamizi wa matukio. Sidhani kama hata kufundishwa kutumia kamera kama kufanya kumbukizi wanafundishwa. Ni nadhari ya utalii ni nini.. lakini hawajui namna gani watatangaza utalii wenyewe. Ninajua kwa sababu marafiki zangu wako huko, najua kwa sababu ninaona matukio mengi yakitokea lakini mamlaka za utalii hazionekani. Najua kwa sababu mimi mwenyewe niko najihusisha na uwekaji kumbukumbu za mambo ya utalii na hakuna kati ya watendaji wako mwenye taarifa za kutosha.
Nikueleze Mheshimiwa Rais kama kuna mtu anapiga picha za ndege kwa ajili ya utalii, basi atakuwa mzungu na ndivyo ilivyo kwa wanyama. Lakini tuna vyuo vya utalii, vya uandishi wa habari, ya wanyamapori. Lakini hatuna wataalamu wa kupiga picha zinazohusiana na utalii, ukifika kwenye masoko na biashara huko mimi sijui. Mimi hupiga picha za ndege nikiwa na nia ya kuutangaza utalii, watendaji wananishangaa, na wananchi wenzangu wananishangaa. Hawa ndio wataalamu wetu na hawa ndio wananchi wetu, hawajui chochote kuhusu kuutangaza utalii.
Tunashindwa kuhifadhi vivutio vya utalii. Tunaua wanyama wale wale ambao wanatuletea pato, tena bila kujali, tunakata misitu kama wendawazimu kutafuta mkaa, mito inakauka;Â tukifika mijini nyumba ambazo ni vivutio vya utalii zinabomolewa kwa kisingizo kisojaa maji kwenye kikombe, lakini tunabomoa chochote kwa sababu watendaji hawajui maana ya utalii na kwa sababu ya uvivu wa kukarabati na kwa sababu wananchi hawajui maana ya utalii.
Soko la Morogoro limevunjwa.. kuna soko la 1907 na soko la 1953… Waingereza na Wajerumani. lakini tumevunja. Hakuna sababu ya maana… huko Ulaya wanakotufundisha mambo ya usasa majengo yao ya zamani wameyatunza na wanaendelea.
Mheshimiwa Rais nadhani kuna umuhimu wa kukaa na watendaji na wadau tukajadiliana kwa mapana juu ya namna ya kuukuza utalii. Mawazo yapo, fedha hakuna; wenye Mawazo wapo, lakini watendaji hawasikilizi.