23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA VS YANGA SASA KUPINGWA FEBRUARI 18

yanga-na-simba

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

PAMBANO la watani wa jadi mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, umesogezwa mbele kwa siku 13.

Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa Jumapili, Februari 5 mwakani lakini ratiba mpya iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeusogeza mbele mchezo huo hadi Jumamosi, Februari 18 mwakani.

Wekundu wa Msimbazi ndiyo watakuwa wenyeji wa pambano hilo linalotarajiwa kuwa la kukata na shoka, ikizingatiwa timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza msimu huu.

Yanga watavaana na Simba kwa mara ya kwanza chini ya kocha wake mpya kutoka Zambia, George Lwandamina, ambaye amekabidhiwa majukumu ya Mholanzi Hans van der Pluijm ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema ratiba hiyo imepangwa kwa kuzingatia kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hivyo haitafanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza wa ligi.

“Ratiba ya mzunguko wa pili haitakuwa na mabadiliko kwa sababu imepangwa kwa kufuata kalenda za mechi ya kimataifa, ikiwamo mechi za Yanga ambao watashiriki Klabu Bingwa Afrika na Azam FC kwenye Kombe la Shirikisho,” alisema Lucas.

Alisema ratiba hiyo pia imezingatia Kombe la Mapinduzi iliyopangwa kuanza Januari mosi hadi 13 mwakani.

Katika mechi za ufunguzi wa mzunguko wa pili wa ligi Desemba 17, mabingwa watetezi Yanga watavaana na JKT Ruvu katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Mbeya City ikichuana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Ruvu Shooting watakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Pwani wakati Mwadui FC ikiikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Siku inayofuata, Ndanda FC itaikaribisha Simba katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, Mbao FC itakutana na Stand United kwenye Uwanja wa Kirumba, Mwanza, African Lyon imepangwa kucheza na Azam FC katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Tanzania Prisons ikiialika Majimaji FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles