KIKOSI cha kocha Mauricio Pochettino, klabu ya Tottenham, imekuwa ya kwanza kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa klabu ambazo zinashiriki Ligi Kuu nchini England.
Timu hiyo imeshindwa kuingia hatua ya 16 bora katika kundi lao E, baada ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Monaco ya nchini Ufaransa kwenye Uwanja wa Stade Louis 11.
Katika kundi hilo, Tottenham walikuwa wanatafuta alama tatu kuweza kusonga mbele ambapo wangekuwa na alama saba sawa na Bayer 04, lakini Monaco ambao walikuwa na alama nane kwenye kundi hilo walikuwa hawana sababu ya kushinda kwa kuwa tayari walikuwa wameweza kufuzu hatua ya 16 bora.
Kocha wa klabu ya Tottenham, Pochettino, ameweka wazi kuwa kutolewa kwenye michuano hiyo kumetokana na kuwa na wachezaji wenye kiwango cha chini.
Pochettino amedai kuwa lazima ajipange vizuri kwa ajili ya kuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao wataweza kupambana na kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Kikosi hicho kina wachezaji wenye majina makubwa kama vile Harry Kane, Dele Alli, Christian Eriksen, Moussa Sissoko, Mousa Dembélé na wengine wengi, lakini walishindwa kuonesha uwezo wao ndani ya dimba hilo.
“Kwa miaka miwili na nusu tumekuwa tukibadilika kwa kiasi kikubwa na tumeweza kupunguza nafasi ambazo tulikuwa tunaachwa na klabu nyingine, kwa sasa tuna furaha kwa kuwa bado tunashindana kwenye ligi kuu, ni wazi kwamba kushindana sehemu mbili kubwa ni kazi sana na inahitaji maandalizi makubwa.
“Ninaamini kwamba klabu hii inahitaji wachezaji wenye uwezo mkubwa, kwa sasa tuna wachezaji bora ambao wanaweza kuleta ushindani mkubwa ndani ya ligi kuu ila tumeshindwa kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa kutokana na kuwa na wachezaji ambao ni majeruhi.
“Hadi sasa hatujafungwa hata mchezo mmoja kwenye ligi kuu na tunakaribia kwenye nafasi ya juu, tumeshindwa kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa, lakini tumejifunza kitu na sasa tunatarajia kupambana kwa ajili ya ligi kuu,” alisema Pochettino.
Michezo mingine iliyopigwa juzi ni pamoja Borussia Dortmund ambao walishinda mabao 8-4 dhidi ya Legia Warsaw na kuvunja rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa kufungana jumla ya mabao 12.
Mabingwa Licester City walishinda mabao 2-1 dhidi ya Club Brugge na kuwafanya mabingwa hao wa England kuongoza kundi G wakiwa na alama 13 wakifuatiwa na FC Porto wenye alama 8.
Matokeo mengine ni pamoja na Sporting ikipokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Real Madrid, CSKA Moscow ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya Bayer 04 Leverkusen, FC Copenhagen ikitoka bila kufungana dhidi ya FC Porto, huku Dinamo Zagreb ikipigwa bao 1-0 dhidi ya Olympique Lyonnais wakati huo Juventus ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Sevilla.