MIONGONI mwa maneno ambayo Rais John Pombe Magufuli amekuwa akiyasema na kuyarudi mara kwa mara ni yale yanayoonesha nchi ilikuwa ina mambo ya hovyo hovyo. Amekuwa akiyasisitiza kwa kuonesha kuwa mambo hayo yalikuwa yanaudhi na kulidhihaki kundi fulani la watu.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari hivi karibuni alipoulizwa masuala kadhaa ndipo aliposema kuwa jukumu alilonalo hivi sasa ni kuhakikisha kuwa anainyoosha nchi kwanza na mambo mengine yatafuata.
Kwa kutafakari kirahisi tu ni kwamba ameiona nchi hii kwamba ilikuwa imetumbukia katika janga la kulea baadhi ya mambo ambayo yaliwahi kuainishwa na waasisi wa Taifa hili na hususani kumea na kustawi kwa janga la rushwa iliyokomaa pamoja na vitendo vya ufisadi.
Inapoainishwa mifumo ya uendeshaji wa huduma za kijamii kinachojidhihirisha ni kwamba jamii ilishajengeka katika matabaka ambayo mara zote yanakuwa ni mawili ya wavuja jasho na wavuna jasho.
Ilishakuwa rahisi kuaminishwa kuwa baadhi ya sehemu za kutoa huduma za jamii kwamba ziligeuzwa kuwa ni mapango ya uporaji na utukufu wake ulishadhoofu na kwamba njia ya kuzifikia huduma hizo zilikuwa zimejaa miiiba na zilikuwa hazipitiki.
Inaweza kuelezwa hivyo kutokana na ukweli kwamba miguu ya wavuja jasho iliyopeku haingeweza kumudu kupita na kuzifikia. Lakini ni nani aliyejali hali hiyo ya mvuja jasho?
Taswira inayojitokeza hapo ni kwamba lilishajengeka pengo katika ya makundi hayo mawili, na hivyo kuwapo dhana ya kudharauliana, kupuuzana na hata kudhihakiana kutokana na kuwapo kwa tofauti hiyo.
Ukweli mwingine ni kwamba wakati wavuna jasho wakiwa wanapanda ngazi wavuja jasho walikuwa wanashuka ngazi kuelekea ndani ya dunia ya umaskini na hivyo taswira hiyo inaonesha wazi kwamba kati ya wawili hawa hawawezi kushikana mikono. Hilo ni jambo lisilowezekana kwa mpanda ngazi na mshuka ngazi kushikana mikono.
Macho ya wavuja jasho yanapoangalia mambo yanayojitokeza kwa sasa hata kama hayatawafurahisha wengine kwa upande wa pili wapo watakaokuwa wanaoona ahueni kutokana na dhihaka iliyokuwa imekithiri.
Yapo baadhi ya mambo ya kawaida tu ambayo kila wavuja jasho wanapokumbana nayo huwa wanaamini kweli aliye juu msubiri chini atashuka tu. Lakini awali ilikuwa aliye juu mfuate huko huko. Hatashuka.
Hivi sasa wavuja jasho wameanza kuiamini ile kanuni ya Kifizikia ya mvutano kwamba huko wavuna jasho walikokuwa wanaelea hawawezi wakadumu huko lazima watashuka kwa kuwa manyoya ya mabawa yao yameanza kupukutishwa.
Inapoelezwa kuwa wavuna jasho hivi sasa wanajifunza kozi ya kuishi maisha kwa kuvuja jasho na uzoefu wanautafuta kutoka kwa wavuja jasho ambao wamebobea katika kuishi kwa jasho lao miaka nenda rudi ndipo hapo inajionesha kuwa heshima inarudi.
Zilikuwapo kauli za kukufuru kwamba kutokana na kuvimbiwa jasho walilolivuna na kuwajengea hofu wavuja jasho, ilikuwa ni rahisi kuzisikia kama vile “unajua mimi ni nani?” na nyingine nyingi ambazo zilitokana na jasho walilovuna kuwa limewakifu.
Kile kinachojulikana kwamba walikuwapo wavuna jasho ambao katika sehemu nyingine za huduma walikuwa na vigoda vyao maalumu na hakuna aliyeruhusiwa kukalia vigoda hivyo ni kwamba hivi sasa vinajulikana kama ni vigoda vya moto hawamudu tena makeke ya kuvikalia. Hilo ndilo linamfanya mvuja jasho achoke na kulegea mwili.
Lakini ukweli unabakia kuwa ukiona mambo yanaenda hivyo jua kwamba utafika wakati ambao licha ya baadhi kutoamini au kukubaliana na mwenendo wa kuinyoosha nchi wavuna jasho watafumbuka macho na kuona na kukiri kuwa walivuna jasho la wavuja jasho na watawapa heshima inayostahili.