Na AMINA OMARI-TANGA
TANZANIA ina vituo vya afya 440 pekee licha ya utekelezaji wa sera ya afya kutiliwa mkazo katika maeneo mengi nchini.
Kutokana na uhaba huo, serikali imesema iko kwenye mchakato wa utekelezaji wa ujenzi wa vituo hivyo katika kila kata nchi nzima kumaliza changamoto hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo alisema hayo jana kwenye ziara yake wilayani Pangani.
Alisema mpango huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka ujao wa fedha kwa kila halmashauri kujengewa kituo kimoja cha afya katika ngazi ya kata.
“Kupitia mpango huo serikali itaweza kwa kiasi fulani kufikia lengo lake iliyojiwekea la kila kata kuwa na kituo cha afya kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah alisema wilaya hiyo ina kata 14 lakini ina kituo cha afya kimoja hali inayosababisha changamoto ya utoaji wa huduma.