WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amesema sekta ya utalii nchini inapaswa kupewa kipaumbele zaidi kwa kuwa inaingiza mapato ya Sh bilioni mbili kwa mwaka.
Amesema kiwango hicho kinachopatikana ni kidogo kwa kuwa Tanzania haijaweza kutumia kwa ukamilifu fursa zote katika sekta hiyo.
Profesa Maghembe alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wanafunzi, wahitimu na wazazi katika mahafali ya sita ya Chuo cha Hoteli na Utalii Njuweni mjini Kibaha.
“Sekta ya utalii nchini ni muhimu kwa kuwa inagusa jamii kwa kupitia fursa za ajira. Hivyo basi, Serikali bado inaendelea kuweka mipango mizuri zaidi ya kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuheshimiwa nje na ndani ya nchi.
“Pia, kuna haja kwa Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio vya utalii hivyo waweze kujifunza mambo muhimu yaliyopo katika utalii.
“Sekta hii ya utalii ni muhimu kwetu sote kwa kuwa imekuwa sehemu ya kutoa ajira kwa Watanzania kupitia hoteli na hata vivutio mbalimbali,” alisema.
Waziri alisifu jitihada za Hoteli ya Njuwen kwa kuwa ni taasisi inayofanya kazi kwa kushirikiana na Serikali katika kukuza utalii.
Aliwataka walimu kutumia mitaala mizuri ya kufundishia kuipa heshima sekta ya utalii nchini.
Mkuu wa Chuo hicho, Nditi Rashid, alisema pamoja na mafanikio yaliyopo bado chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa vya teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Kwa hiyo, tunakuomba mheshimiwa waziri utusaidie kupata vifaa hivyo tuweze kwenda sawa na teknolojia iliyopo duniani kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo kwa njia ya mtandao.
“Ninasema hivyo kwa sababu mpango wa chuo chetu ni kujenga chuo cha kisasa kitakachogharimu Sh bilioni sita na chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 3000 kwa wakati mmoja,” alisema Rashid.