Rais mteule wa Marekani Donald Trump aliwashangaza wateja, na wanahabari wanaofuatilia safari zake, baada ya kujitokeza kwa kushtukiza katika mgahawa mmoja New York.
Wanahabari waliopewa kazi ya kufuatilia safari zake walibaki kushangaa kwani walikuwa wameelezwa kwamba angesalia nyumbani jioni hiyo.
Lakini badala yake, aliandamana na kundi dogo la maafisa hadi kwenye mgahawa wa 21 Club katika mtaa wa Manhattan, mmoja wa migahawa anayoipenda sana.
Video zilizopigwa wakati wa kisa hicho zinamuonyesha Rais Trump akiwasalimia wateja na kuwaambia kwamba atapunguza kodi wanayolipa kwa serikali.
Hatua ya kutofuata desturi na kutowafahamisha wanahabari wanaomfuatilia rais mteule kuhusu safari hiyo imevitia hofu vyombo vya habari Marekani.
Msemaji wa Trump, Hope Hicks baadaye aliwaambia wanahabari kwamba hakufahamu mipango ya Rais Trump na akawaahidi wanahabari kuwa watapata uhuru wa kufikia maafisa wa serikali na taarifa za serikali kama ilivyokuwa chini ya marais wengine.
Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya White House kimeshutumu kisa hicho. Viongozi wa chama hicho wamesema “haikubaliki kwa rais ajaye wa Marekani kusafiri bila waandishi wa habari wa kufuatilia habari zake na kuwafahamisha wananchi kuhusu alipo”. Source: BBC Swahili