25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI yalia na upotoshwaji ‘mtoto wa betri’

Profesa Mohamed Janabi
Profesa Mohamed Janabi

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SIKU chache tangu kutokea kifo cha mtoto Happiness Josephat (6), aliyekuwa amefanyiwa upasuaji wa kupandikizwa betri ndani ya moyo wake, hali ya wasiwasi imetanda miongoni mwa wagonjwa waliopandikizwa kifaa hicho.

Wasiwasi huo umetanda kutokana na taarifa zinazosambazwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, watumiaji wa mitandao hiyo wakidai kifo hicho kimesababishwa na kifaa hicho kushindwa kufanya kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba ni za upotoshaji.

“Kwanza jamii ielewe kwamba, JKCI tumesikitishwa mno na kifo cha Happiness kwa sababu tulikuwa tukifuatilia maendeleo yake kwa ukaribu, na kifo chake kimetushtua kwani kimetokea ghafla.

“Baada ya kifo kile kumekuwa na taarifa nyingi zinazosambazwa mtandaoni ambazo si sahihi na zimepelekea wagonjwa wetu tuliowafanyia upasuaji wa aina hiyo kuwa na hofu na wasiwasi.

“Ukweli ni kwamba kifaa kile tulichomuwekea hakikuwa na tatizo lolote, kilikuwa kinafanya kazi sawa sawa nah ii ni kwa mujibu mama yake, Elitruda Malley ambaye tulihojiana naye kujua alipatwa na shida gani.

“Akatueleza kuwa alianza kulalamika kuwa anasikia maumivu ya tumbo, akachukua kifaa cha kupima mapigo ya moyo ambacho tulimpatia, alipompima kifaa kilionesha kuwa yalikuwa sawa sawa.

“Lakini akatueleza bado mtoto alilalamika tumbo linamuuma, akampeleka hospitali ya Selian lakini hawakugundua tatizo na wakampatia dawa ya diclofenac kutuliza maumivu,” alisema.

Profesa Janabi alisema hata hivyo tatizo hilo liliendelea ambapo mama huyo alimrudisha tena mwanawe hospitalini hapo kwa uchunguzi zaidi.

“Lakini bado tatizo halikuonekana, na alipokuwa akipimwa mapigo ya moyo kifaa kilikuwa kinasoma yapo sawa sawa, ripoti ya awali ya madaktari wa selian inaeleza kuwa alisumbuliwa na tumbo, tumeomba watupatie uchunguzi ufanyike kwa kina na watupatie taarifa kamili,” alisema.

Dk. Janabi alisema wanataka kufanya uchunguzi zaidi kwani hadi sasa jumla ya wagonjwa 31 wamefanyiwa upasuaji wa kupandikizwa kifaa na wanaendelea vizuri pasipo shida yoyote.

“Happiness ndiye mtoto wa kwanza nchini kuwekewa kifaa hiki ndiyo maana tulisema ni upasuaji wa kihistoria, tumesikitishwa mno na kifo chake, taarifa zetu zinaonesha alizaliwa Desemba 16, 2012 huko Mbulu, Manyara na Julai 15, mwaka huu tulimfanyia upasuaji wa kumpandikiza kifaa hicho baada ya kugundulika kuwa alizaliwa na tatizo lijulikanalo kitaalamu ‘heart break’.

“Mfumo wa umeme wa moyo wake haukuwa unafanya kazi sawa sawa kama inavyotakiwa, ndio maana mapigo yake yalikuwa kati ya mara 20 hadi 25, madaktari wa JKCI tulifanya upasuaji huo kwa kushirikiana na wenzetu wa marekani na aliruhusiwa wiki mbili baadae, Agosti mosi, mwaka huu.

“Tulitamani hata tungeweza kuufanyia mwili wake ‘postmotum’, ili tujue nini hasa kimesababisha kifo chake ikiwa kifaa tulichomuwekea kilikuwa kinasoma mapigo ya moyo vizuri,” alisema.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu, Elitruda alisema amesikitishwa na taarifa zinazoenezwa mtandaoni kwani si za kweli.

“Mwanangu akuugua kifua, bali tumbo na alikuwa anatapika, kifaa kilikuwa kizima.. mimi ni muelewa, ni muuguzi,  alinifia mikononi mwangu, nasikitishwa na uzushi huo wa mtandaoni,” alisema.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Moyo Idara ya Watoto, Edwin Sharau alisema kila mwaka duniani watoto 22,000 huzaliwa na tatizo kama alilokuwa nalo marehemu Happiness.

“Takwimu zinaonesha Tanzania kwa mwaka huzaliwa mtoto mmoja, hali hiyo hutokea pale nguvu ya kupigana na magonjwa ya mama wakati wa ujauzito ‘antibody’ zinapovuka kwenye kondo la mama kisha kuingia kwa mtoto akiwa tumboni.

“Asilimia 70 ya watoto wanaokumbana na nguvu hiyo, hufariki dunia, asilimia 25 huzaliwa lakini hufariki katika miezi ya kwanza na asilimia 85 kati ya hawa asilimia 25 ambao huzaliwa hufariki kwa sababu moyo wao hushindwa kufanya kazi ipasavyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles