32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa JPM: Nilifikishwa Muhimbili nikiwa sijitambui

janeth-magufuli

Na MWANDISHI WETU  

MKE wa Rais John Magufuli, mama Janeth, amesema alifikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiwa hajitambui.

Mama Janeth, ambaye alifikishwa hospitalini hapo Novemba 9, 2016, aliyasema hayo jana kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.

Kwa mujibu wa taarifa hayo, mama Janeth alitoa kauli hiyo  muda mfupi baada ya kuruhusiwa kuondoka katika Wodi ya Sewahaji,  alikokuwa amelazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

“Namshukuru sana Mungu kwamba afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru madaktari na wauguzi, nimepata huduma nzuri sana maana siku nilipoletwa hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya, lakini mmenipigania na leo (jana) narudi nyumbani nikiwa na afya imara,” alisema.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kinachomsumbua mama Janeth, zaidi ya yeye mwenyewe kuwahakikishia Watanzania kwamba, kwa sasa yupo vizuri kiafya, baada ya kupata matibabu.

Alisema madaktari wamemtaka kumalizia matibabu yake akiwa  nyumbani.

 “Naomba pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishia kuwa sasa nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani, ambako nitamalizia matibabu yangu,” alisema.

Itakumbukwa mama Janeth alifikishwa na kulazwa hospitalini hapo baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.

Awali, MTANZANIA lilizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha, ambaye alisema mama Janeth aliruhusiwa saa tatu kasoro asubuhi.

“Madaktari wake walimpima na kuona kuwa anaendelea vizuri, kwa hiyo wamempatia ruhusa baada ya kujiridhisha na mwenendo wa afya yake,” alisema Aligaesha.

Siku ambayo mama Janeth alifikishwa hospitalini hapo watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia MTANZANIA Jumamosi kuwa, kulikuwa na ulinzi mkali, huku madaktari na wauguzi wakionekana kuhaha kuokoa maisha yake.

Juzi saa 7:00, muda ambao umewekwa kwa ajili ya kuwaona wagonjwa, Rais Magufuli akiwa na msafara wake alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kumjulia hali mke wake.

Fursa hiyo aliitumia pia kuwasabahi wagonjwa wengine ambao wamelazwa katika wodi hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa mtu mwenye hadhi ya mke wa rais kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka hospitalini humo, wamekuwa wakipokea viongozi mbalimbali pamoja na wake zao, miongoni mwao wakiwa ni wale wanaopata matibabu na kuruhusiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles