Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph Mkirikiti amewataka wananchi kuzalisha mafuta ya alizeti, ufuta na nazi kwa wingi ili kujiongezea kipato na ajira ya kudumu.
Mkirikiti aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa vitendo kwa wakulima ambao ni wazalishaji wa bidhaa za mbegu za mafuta ya ufuta, nazi na alizeti wa Ruangwa Pamoja na hilo, alipokea pia lebo za vifungashio vya mafuta ya alizeti kwa wazalishaji wa bidhaa za mafuta ya alizeti zaidi ya 1,000 zilizotengezwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).
Alisema mafunzo hayo ya siku nne yatasaidia kuwawezesha kufahamu namna bora ya kupata bidhaa za mbegu za mafuta ya ufuta, alizeti na nazi, kuwa na lebo bora kwenye kila bidhaa inayozalishwa.
Hata hivyo, Mkirikiti aliongeza kuwa ana imani wananchi wa Ruangwa na Masasi watajifunza namna ya kuboresha ubora wa bidhaa na mbinu ya kuuza bidhaa hizo kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Elimu mtakayopata hapa itawachukueni kwenye hatua nyingine ya kufanya maboresho makubwa ya ajira yenu, hapa nchini mahitaji ya mafuta ya kula kwa mwaka ni lita 350,000 wakati uzalishaji kwa sasa ni asilimia 40 pekee na asilimia 60 huagizwa kutoka nje ya nchi hivyo basi, tuna fursa kubwa ya kunufaika na sekta hii,” alisema Mkirikiti.
Naye , Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendelo ya Tanzania (TanTrade), Edwin Rutageruka alisema wameandaa mafunzo hayo kwa ushirikiano wa wadau wa kimkakati ili kuimarisha fursa kwa wakulima kuzalisha kitu cha thamani na kuweza kuleta ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.