NA JUSTIN DAMIAN, MAREKANI
TIMU ya kampeni ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump, imekana tuhuma za mgombea wao kuwa na uhusiano na benki moja ya Urusi.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, jarida la Slate la hapa Marekani lilichapisha taarifa za kuwapo kwa mawasiliano ya muda mrefu kwa njia ya mtandao kati ya benki moja kubwa ya Urusi inayojulikana kama, Alfa Bank na taasisi za mgombea huyo.
Jarida hilo lilieleza kuwa, wadukuzi wa mtandao (hackers) waliopo Urusi wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mawasiliano ya barua pepe ya wagombea Urais wa Marekani kupitia mitambo ya kuhifadhia kumbukumbu (servers) na walifanikiwa kukuta server ya Trump ikiwa imeunganishwa na server iliyokuwa na taarifa za benki ya Alfa ya Urusi
Wataalamu wa masuala ya usalama wa mitandao wa Marekani ambao hawakupenda kutajwa majina yao, waliliambia jarida la Slate kuwa mawasiliano yaliyonaswa yanaonekana kuwa ni ya kati ya mtu na mtu na yalifanyika muda wa kazi kwa saa za Marekani na Urusi.
“Watu hao wawili walikuwa wakiwasiliana kwa siri. Neno walilokuwa wanalitumia kufanya mawasiliano yao lilikuwa ni ‘usiri’ na hili limefanyika kwa muda mrefu,” alisema mmoja wa wataalamu hao.
Benki hiyo ilipofuatwa kuulizwa juu ya suala hilo na waandishi wa gazeti la The News York Times, mawasiliano hayo yalisitishwa.
Hata hivyo, msemaji wa kampeni za Trump, Hope Hicks, alikana kuwepo kwa mawasiliano yoyote kwa njia ya mtandao kati ya taasisi ya mgombea wao na benki hiyo ya Urusi.
Server hiyo ya barua pepe ambayo ni maalumu kwa ajili ya shughuli za masoko na ambayo inatumiwa na mtu asiyekuwa mwajiriwa wa benki hiyo (third party), moja kwa moja haikuwahi kutumika tangu mwaka 2010.
“Hakuna taasisi yoyote ya Trump inayotuma au kupokea taarifa zozote kutoka kwenye server inayotajwa. Ni vyema ikafahamika kuwa hakuna taasisi ya mgombea wetu yenye uhusiano wa aina yoyote na taasisi ya aina yoyote ya Urusi,” alisema msemaji wa Trump.
Suala la Trump kuwa na uhusiano na Russia ambaye ni hasimu wa Marekani, limekuwa likizua mjadala hapa Marekani. Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani, James Comey, amekuwa akisita kulizungumzia suala hilo ingawa lina ukweli ndani yake.
Seneta anayewakilisha kundi la wachache (minority) katika Bunge la Marekani, Harry Reid, Jumapili wiki iliyopita alimwandikia Comey akimshutumu kushikilia taarifa za Trump kuwa na uhusiano na Urusi
Tarehe 7, Oktoba mwaka huu, Idara ya Usalama wa Ndani na Ofisi ya Usalama wa Taifa ya hapa Marekani ilitoa taarifa ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani, lakini boss huyo wa FBI hakutaka taasisi yake itajwe kuhusika na taarifa hiyo.