29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu, Lema matatani

lema-na-lissu

JANETH MUSHI ARUSHA Na KULWA MZEE, DAR

JESHI la Polisi nchini, limemkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), akiwa mjini Dodoma na kumsafirisha usiku hadi jijini Arusha.

Lema, aliyekuwa anahudhuria vikao vya Bunge, alikamatwa saa chache juzi usiku, baada ya kuahirishwa kwa vikao vya Bunge.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliithibitishia MTANZANIA juu ya kukamatwa kwa mbunge huyo kwa ajili ya mahojiano ya tuhuma zake za uchochezi dhidi ya Rais, Dk. John Magufuli.

“Tunamshikilia Lema na hatutampa dhamana mpaka tumalize kumhoji. Kuna masuala tulikuwa hatukumhoji juzi na akimaliza kuhojiwa leo (jana), tutampeleka mahakamani,”alisema Mkumbo.

“Baadhi ya maneno ya kichochezi ni yale aliyosema kwamba, mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiendelea kugandamiza dekomrasia kwa siasa za ugandamizaji, Taifa litaingia katika umwagaji wa damu.

“Lema alisema pia kwamba, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa kidikteta huku akiwataka wananchi wawe tayari kwa lolote na waache kabisa uoga kwani uoga ni dhambi mbaya kuliko dhambi zote duniani,” alisema Kamanda Mkumbo.

Kukamatwa kwa Lema, ni mwendelezo wa kukamatwa kwake baada ya kufanyiwa hivyo Novemba mosi mwaka huu na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Arusha kwa tuhuma hizo.

Baada ya kukamatwa na kuhojiwa kwa tuhuma hizo Novemba mosi, aliachiwa huru kwa dhamana kwa kuwa jadala la suala lake lilipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi za kisheria.

Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeamuru Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), akamatwe baada ya kushindwa kutii dhamana.

Mahakama hiyo, pia imeamuru wadhamini wa  Lissu waitwe ili kujieleza kwanini wasilipe fungu la dhamana walilotia saini ambalo ni Sh milioni 10 wakati wanamdhamini Lissu.

Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, wakati wa kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kutokana na Lissu kushindwa kufika mahakamani hapo, huku mdhamini wake, Robert Kapula, akidai mteja wake yuko jijini Mwanza kusikiliza kesi.

Kabla ya agizo hilo kutolewa na mahakama, Wakili wa Serikali, Patrick Mwita, alidai mahakamani, kwamba kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo, washtakiwa walipeleka rufani Mahakama Kuu.

“Mheshimiwa hakimu, kutokana na mshtakiwa kushindwa kufika mahakamani, naomba mahakama yako tukufu itoe hati ya kumkamata Lissu ambaye hayupo hapa,” alidai Mwita.

Baada ya kauli hiyo, Hakimu Simba naye alionyesha kushangaa na mahudhurio ya Lissu mahakamani hapo na kuhoji ni kwanini anasafiri bila kuomba ruhusa.

“Kwanini hakuomba ruhusa na kwa sababu gani mahudhurio yake yamekuwa ni matatizo. Hapa kuna misingi ya busara, tungeiangalia vizuri. Hati ya kumkamata Lissu itolewe na hakuna msamaha na hati ya wito itolewe kwa wadhamini waje kujieleza kwanini wasilipe fungu la dhamana,” aliamuru Hakimu Simba.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21, mwaka huu, itakapotajwa tena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles