Na VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) ipo tayari kuanza kufanya upasuaji wa upandikizaji wa vifaa vya kusaidia usikivu kwa watoto waliozaliwa na tatizo la ukiziwi.
Upasuaji huo utaanza kufanyika Desemba, baada ya wataalamu saba waliokwenda kujifunza jinsi ya kufanya upasuaji huo kurejea nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio waliyoyapata ndani ya uongozi wa mwaka mmoja wa Rais Dk. John Magufuli.
“Tulipeleka wataalamu saba wa kupandikiza kifaa cha usikivu kwa watoto na watu wazima, wamerejea wiki iliyopita, upasuaji utaanza Desemba, mwaka huu,” alisema.
Alisema pamoja na hayo, hospitali hiyo imeendelea kutekeleza lengo la Serikali la kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kufuata huduma za kibingwa.
“Kwa kuwekeza huduma za kibingwa, tutasaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali zilizokuwa zikitumika kutibia nje, kwa mfano gharama ya kupandikiza kifaa cha usikivu kwa watoto na watu wazima ni kati ya Sh milioni 60 hadi 100 kwa mtu mmoja, na huduma hii ikianza hapa nchini itasaidia kupunguza gharama hizo,” alisema Aligaesha.
Alisema wataalamu wa upandikizaji figo nao wanatarajiwa kurejea nchini mwishoni mwa mwaka huu na Januari mwakani wagonjwa wa figo wataanza kuhudumiwa nchini.
“Tumeshaanza kuandaa mazingira mazuri, tumepanga kuongeza vitanda vitakavyotumika na watu wanaokuja kuchuja damu kutoka 17 vya sasa hadi 50.
“Gharama ya uchujaji damu nayo imepungua kidogo kutoka Sh 250,000 hadi 170,000, hivyo wakirudi maana yake ni kwamba itapungua zaidi na hivyo kuwapunguzia mzigo wananchi,” alisema Aligaesha.