26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Afrika imefanya maboresho kiuchumi, juhudi inatakiwa ufanyaji biashara

sandton-city-2NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM.

RIPOTI ya uchumi ya mwaka huu ya Benki ya Dunia iliyotolewa mwishoni mwa wiki, imesema kumekuwa na maboresho kwa upande wa mazingira rafiki ya kuvutia wafanyabiashara na wajasiriamali.

Katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA), nchi 37 kati ya 48 zimefanya mabadiliko na kufanya maboresho katika maeneo ya kiuchumi  ambayo ni ongezeko la asilimia 14 ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka juzi.

Baadhi ya nchi zilizokuwemo katika orodha ya kumi bora zenye maboresho hayo ni pamoja na Nigeria, Rwanda, Afrika Kusini, ambazo zimefanya mabadiliko katika sera za uanzishwaji biashara na nyingine ni Cameroon ambayo imeboresha mfumo mzuri wa kuwezesha makampuni ambayo yana matatizo kifedha.

Ripoti imezitaja nchi zilizoshika nafasi za mwanzo duniani katika nyanja ya utendaji bora biashara, zikiwa ni pamoja na  New Zealand na Singapore zilizoshika nafasi ya pili, zikifuatiwa na  Denmark, Hong Kong SAR, China, Jamhuri ya Wananchi wa Korea, Norway; Uingereza, Marekani, Sweden; na iliyokuwa Jamhuri ya watu wa  Yugoslav ya  Macedonia.

Mauritania imetajwa kuleta mabadiliko ya maboresho katika sera za kiuchumi kati ya mataifa 137 hasa kwenye matumizi ya kieletroniki kwa uingizaji wa taarifa za uendeshaji biashara kwa njia hizo za kisasa na hivyo kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa nchi za nje na wale wanaoingiza bidhaa nchini humo.

“Ingawa kumeonekana kuwepo kwa mabadiliko kwa kasi barani Afrika, hasa katika biashara, bado juhudi zinatakiwa zaidi katika kuboresha zaidi mazingira ya ufanyaji biashara kwa kuhakikisha mazingira rafiki yanakuwa endelelvu, hasa kwa wafanyabiashara wadogo na jamii kwa jumla,” anasema Meneja Miradi ya Kibiashara wa Benki ya Dunia katika ripoti hiyo.

Anaongeza kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu uliopita, mabadiliko ya aina hiyo yalifanyika katika nchi 17 zilizo wanachama wa OHADA; ambayo ni Jumuiya  ya Utengamano wa Sheria za Kiuchumi Afrika kwa nchi 17 za Afrika Kati na Magharibi iliyofanywa na nchi 17 kule Port Loius Mauritius Oktoba mwaka 1993.

Nchini Tanzania juhudi zinafanywa na utawala wa awamu ya tano ambapo Rais John Magufuli alisema Serikali yake imejipanga kuwasaidia na kuwaunga mkono wawekezaji wote wa ndani, watakaoanzisha viwanda nchini, ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.

Aidha, alimwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kuhakikisha anatengeneza mazingira yatakayowapunguzia kodi wawekezaji wa ndani na kupandisha kodi zaidi kwa bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi.

Anasema uwekezaji katika sekta ya viwanda ukikua nchini, wakulima wa pamba, korosho, kahawa na mazao mengine ya biashara watazalisha kwa wingi na kupata faida kwa kuwa watakuwa na soko la uhakika, lakini pia viwanda hivyo vitatengeneza ajira na kuuza bidhaa hiyo kwa bei ambayo Watanzania wataimudu.

Anasema Serikali yake imejipanga kuwaunga mkono wawekezaji wazalendo watakaoanzisha viwanda na nguvu kubwa imeelekezwa katika uwekezaji wa viwanda vya uzalishaji utakaotumia kwa wingi malighafi zinazozalishwa nchini.

Dk. Magufuli anasema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020, kupitia sekta hiyo ya viwanda ichangie katika Pato la Taifa kwa asilimia 40 na ajira zitakazozalishwa kupitia viwanda pia zifikie asilimia 40.

“Naamini jambo hili linawezekana kwa sababu nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali zinazowezesha kujenga uchumi wa viwanda, tunayo ardhi ya kutosha, nguvu kazi, misitu, samaki kupitia uvuvi, soko la uhakika kwa kuwa tumezungukwa na nchi zisizo na maji,” anasema rais.

Kwa upande wa suala la utitiri wa tozo kwa wawekezaji viwanda, Dk. Magufuli alieleza kuwa Serikali imeshaunda kamati ya kitaifa kwa ajili ya kuangalia mazingira ya tozo na endapo kutakuwepo  na  zisizo na tija zitaondolewa.

“Ni kweli nchi yetu ina vikodi vingi hasa kwenye mazao kama vile kahawa, pamba na korosho na ninafahamu kuna kodi nyingine ni kwa ajili ya kuliwa na baadhi ya watu, hizi nitaziondoa. Ndiyo maana wengine wananiita mkorofi lakini ninasimamia haki na si jingine,” anasema.

Waziri Mwijage anasema Serikali imeanza kuonesha kwa vitendo dhima yake ya kuijenga Tanzania ya viwanda kupitia Mpango wake wa Maendeleo wa miaka mitano 2016/17 hadi 2020/25.

Kwa upande wa nchi kumi bora duniani zinazoendelea na maboresho hayo kwa kuzingatia mabadiliko yalipofikia ni, Brunei Darussalam, Kazakhstan, Kenya, Belarus, Indonesia, Serbia, Georgia, Pakistan, Umoja wa Falme za Kiarabu  (UAE) na Bahrain.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles