Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
BAADHI ya Wakazi wa Kibamba CCM, wilayani Ubungo, Dar es Salaam, wamelalamikia hatua ya Serikali kubomoa nyumba zao huku wakijua kwamba hazikuwa kwenye mpango huo.
Wakazi hao walisema kuwa kabla ya hatua ya utekelezaji wa bomoabomoa hiyo, Serikali ilitoa taarifa kuwa wataalamu wake walitarajiwa kufika kwenye eneo hilo ili kuweka alama za X kwa nyumba zilizokuwa zinatakiwa kubomolewa.
Wakizungumza na MTANZANIA jana, walisema wanakilaani kitendo kilichofanyika na kukiita cha uonevu ambacho hawatausahau milele.
“Unajua mwandishi baadhi yetu jana (juzi), tumelala hapa hapa kwa ajili ya kulinda baadhi ya mali zetu ambazo zimenusurika kwa uchache, unajua eneo hili ni la kibiashara,” alisema mmoja wao.
Mmoja wa mashuhuda, aliyejitambulisha kwa jina moja la Shabani, alisema operesheni hiyo iliendeshwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ambao wakati wote ikiendelea walifanikiwa kudhibiti udokozi wa baadhi ya mali.
Alisema taarifa ambazo wanazo wananchi hao ni kwamba nyumba 110 zinatarajiwa kuvunjwa ambapo hadi juzi zilizovunjwa hazijafia 50 huku wakitarajia operesheni hiyo kuendelea jana.