SEKTA ya mifugo nchini inakabiliwa na tatizo la kukosekana kwa kiwanda cha kuchakata mazao yatokanayo na mifugo, jambo linalochangia sekta hiyo kushindwa kuchangia pato kubwa la taifa na kushindwa kuwanufaisha wafugaji.
Pamoja na hali hiyo, Serikali imesema iko tayari kushirikiana na wadau wa maendeleo hapa nchini ikiwemo mifuko ya hifadhi ya jamii katika kuanzisha kiwanda cha ngozi katika machinjio ya Sakina ( Arusha Meat), yaliyopo jijini Arusha.
Hayo yalisemwa juzi na Naibu Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha, wakati alipotembelea machinjio hayo kujionea hali ya uzalishaji pamoja na kutembelea soko kuu la Arusha kuona hali ya biashara ya nyama.
“Serikali ya awamu ya tano inatoa msukumo wa kuwa Tanzania yenye uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda hasa vinavyotumia malighafi zinazozalishwa hapa nchini, ila sekta ya mifugo ina changamoto kubwa haina viwanda vya kutosha vya kuchakata mazao na kuongezea thamani.
“Kwa kushirikiana na DC, angalieni namna mnavyoweza kuwa na kiwanda cha ngozi hapa na wizara yangu iko tayari kufanya mazungumzo na mifuko ya hifadhi za jamii ili kuwashawishi wawekeze katika sekta hii, ili wafugaji wawe na uhakika wa soko, lakini pia mtaongeza mapato na kuweza kujiendesha zaidi,” alisema.
Ole Nasha alisema sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi inategemewa na Watanzania zaidi ya asilimia 75 hapa nchini, hivyo viwanda vitasaidia kukuza uchumi, akitolea mfano nchini Kenya, sekta ya mifugo inaiingizia taifa hilo mapato makubwa kutokana na kuwa na viwanda vingi vya kuongezea thamani mazao yatokanayo na mifugo ikiwemo viwanda vya ngozi.
“Gereza la Karanga la Moshi linatengeneza viatu vizuri sana vya ngozi, ila asilimia kubwa inatoka Kenya, kwa hiyo mkianzisha kiwanda kinachochakata ngozi kuanzia hatua ya kwanza, mtaweza kutengeneza bidhaa bora za ngozi kwani hata hizo zinazotoka Kenya huwa ni mifugo yetu inaenda kuuzwa huko halafu wanatengeneza ngozi na kuja kutuuzia tena,” alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo ya kuchinja na kusindika nyama katika machinjio hayo, Joseph Sunguya, alisema Halmashauri ya Jiji la Arusha imeruhusu bodi ya kampuni kuwekeza katika mradi wa ujenzi na upanuzi wa kitengo cha uzalishaji na usindikaji nyama.
Alisema katika mradi huo utakaogharimu zaidi ya Sh bilioni 3.5 ambao utajumuisha kununua mashine za kisasa, mpaka sasa wamewasilisha andiko la kibiashara kwa benki za NMB na CRDB na kuwa mazungumzo yako katika hatua za mwisho, ambapo wanasubiri uamuzi wa mwisho wa benki hizo.