25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Ziara ya Mfalme wa Morocco yazua maswali

Mfalme Mohamed VI
Mfalme Mohamed VI

NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Mshikamano wa Tanzania na Sahara Magharibi (TASSC), imemtaka Rais Dk. John Magufuli kutoyumbisha msimamo wa kutoitambua nchi ya Morocco  kutokana na kuitawala kimabavu Sahara Magharibi na kuwashikilia wafungwa wa kisiasa wa taifa hilo.

Kauli hiyo imetolewa wakati kiongozi wa nchi hiyo, Mfalme Mohamed VI akitarajia kuwasili nchini leo akiwa na ujumbe wa watu 1,000.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa Idara ya Haki za Binadamu wa TASSC, Alphonce Lusako, alisema kwa miaka kadhaa sasa Tanzania imekuwa ikiunga mkono harakati za Sahara Magharibi kuhakikisha inapatiwa uhuru   na Morocco, hivyo kitendo cha mfalme huyo kutembelea  nchini, kinatia shaka na kudhani kwamba huenda Tanzania ikalegeza msimamo wake katika suala hilo.

“Tunajua Rais Magufuli huwa hayumbushwi na katika hili  nalo tunaamini hatotuangusha, msimamo wa waasisi wetu ni kutoitambua nchi ya Morocco sasa, na ndiyo maana viongozi wake hawajawahi kuja nchini, sasa kama mfalme anakuja kwa masuala ya kibiashara kuna haja ya kuwa waangalifu kama nchi,” alisema Lusako.

Alisema diplomasia ya uchumi isiwe kisingizio cha kuizika misingi ya uhuru, utu, undugu na kuwapigania wanyonge   pamoja na kuyumbisha msimamo wa taifa katika kuiunga mkono Sahara Magharibi.

Mbali na hilo, TASSC pia imesikitishwa na kitendo cha Morocco kuendelea kupuuzia wito wa Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Mataifa (UN) na jumuiya za kimataifa kwa ujumla zinazoitaka nchi hiyo kuipatia Sahara Magharibi haki yake ya kujitawala.

Alisema kamati inamtaka mfalme wa Morocco kuacha mara moja vitendo vya kibeberu vya kuikalia Sahara Magharibi kupewa uhuru wake.

Aliongeza kuwa kamati pia inamtaka mfalme wa Morocco kuacha mara moja vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu  kwenye maeneo inayoyakalia kimabavu, hasa katika maeneo yenye madini ya phosphate na rasilimali bahari na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa wa nchi hiyo.

AZIMIO LA UMOJA WA MATAIFA

Licha ya kuundwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kura ya Maoni Nchini Sahara Magharibi (The United Nations Mission for Referendum in Western Sahara-MINURSO) mwaka 1991 ili kuipatia haki yake ya kujitawala, Morocco imepuuza suala hilo hali ambayo imechochea ukandamizaji pamoja na uvunjaji wa haki za binadamu.

Aidha, uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (International Court of Justice-ICJ) kwenye hukumu yake ya mwaka 1975, unaonyesha kwamba madai ya Morocco juu ya uhusiano wake na Sahara Magharibi, hayakuwa na msingi wowote wa kuinyima haki yake ya kujitawala na kuepuka makucha ya mkoloni mpya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles