Na SAMUEL SAMUEL,
TANZANIA imekuwa na historia nzuri katika mchezo wa ndondi kulinganisha na michezo mingine, ingawa kipaumbele chake bado ni changamoto ambayo inakosa tafsiri makini kupata mustakabali mzuri.
Katika historia ya michezo iliyoweza kulitangaza vema taifa hili kimataifa, ndondi inashika namba moja kwa rekodi na mafanikio mbalimbali ambayo wana masumbwi wamefanikiwa kuyapata, aidha katika mrengo wa ndondi za ridhaa au za kulipwa.
Tukianzia kwenye upande wa ngumi za kulipwa, bondia Rashid Matumla amelitangaza vema taifa hili kuliko hata timu za soka ngazi ya vilabu au timu ya taifa, ukihesabika kama mchezo unaopendwa zaidi.
Rashid, aliyezaliwa mkoani Tanga Mei 6, 1968, aliingia katika masumbwi mwaka 1979 ambapo ameshiriki mashindano mbalimbali kama vile ile ya Olimpiki ya Seoul 1988.
Amewahi kuwa bondia bora Afrika Mashariki na Kati mwaka 1990 na mwaka huo huo alikuwa bingwa wa ridhaa Afrika Mashariki na Kati.
Mwaka 1997 alitwaa ubingwa wa Afrika na kutwaa taji la Mabara linalotambuliwa na WBU mwaka huo huo.
Mwaka 1998 alitwaa taji la kimataifa WBU na mwaka huo huo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU uzito wa light middle.
Amecheza michezo 24 katika ndondi za kulipwa na ameshindwa mara moja. Kati ya hiyo, 14 ameshinda kwa knockout. Historia hii fupi ya ‘Tyson’ huyu wa Tanzania inatosha kukupa picha kamili ya mchezo wa ndondi jinsi ulivyoweza kuitangaza nchi hii kimataifa.
Ubora wa wana masumbwi wa Tanzania uliifanya serikali ya China ikishirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kujenga ulingo wa kisasa wa ndondi ambao serikali imeukabidhi kwa Jeshi la Wananchi Tanzania kama wasimamizi wa ulingo huo.
Hii pia ni alama sahihi ya umuhimu ya mchezo huu nchini na kimataifa.
Mchezo huu wa ndondi chini ya Shirikisho la Ndondi Tanzania (TBF), umekuwa chanzo kizuri cha ajira rasmi kwa vijana mbalimbali ambao wameweza kuitangaza vema nchi hii, ukiondoa kile kizazi cha dhahabu cha akina Matumla.
Mwaka jana Francis Cheka, bingwa wa IBF Afrika na bondia bora hivi sasa Tanzania akihojiwa na waandishi wa habari, aliwahi kusema, kabla ya kujiunga na ndondi alikuwa mzoa taka Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam kujitafutia kipato, lakini kwa sasa anamshukuru Mungu ndondi za kulipwa zinampa ajira, lakini bado haifanyi kusahau historia ngumu ya maisha yake huko nyuma, ndiyo maana amempa mwanawe jina la Historia kama kumbukumbu.
Licha ya mazuri yote haya ya TBF na lile za ngumi za kulipwa (TPBO), bado hawajaupa mustakabali mzuri mchezo huu kufika mbali kimataifa.
Migogoro ya mara kwa mara kati ya mashirikisho hayo mawili yanaufanya mchezo huo kushindwa kustawi vema na kuendeleza historia yake maridhawa nchini.
Ndondi inakosa mapromota wazuri kwa sasa, kutoa fursa kwa vijana wengi kuupenda mchezo huo ili taifa lizidi kujitangaza vema kupitia damu changa kwenye mchezo huo.
Mfano mwanzoni mwa mwezi huu mabondia wa Tanzania walisafirishwa kwa njia ya basi kutoka Tanzania hadi Namibia kushiriki mapambano ya ubingwa, hali iliyowafanya kupanda ulingoni wakiwa na uchovu mwingi na wote kupigwa raundi ya tano na kupoteza mapambano hayo nje ya nchi.
Hii inaonesha mapromota wababaishaji wameivamia tasnia hii na kuharibu mustakabali mzuri wa mchezo huu Tanzania.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT), linahitajika kufanya kazi ya ziada kufufua mustakabali bora wa mchezo huu ili kuendeleza ubora wa ngumi Tanzania, kama ilivyokuwa enzi za akina Rashid Matumla, Stanley Mabesi ‘Ninja’ na wakali wengine kama Francis Miyeyusho.
Mchezo huu umebaki kuendelezwa na timu za majeshi kuliko raia ambao wengi wao wanaunda timu ya taifa ya ngumi za ridhaa. Mikakati iwekwe kuendeleza mchezo huo katika taasisi za kiraia au watu binafsi wenye ari na moyo wa kucheza mchezo huo ambao ndio msingi wa ndondi za kulipwa ambazo kwa kiasi kikubwa zimeweza kulitangaza taifa hili kuliko ndondi za ridhaa.