27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO KABWE: Muswada wa huduma za habari ni hatari

Zitto Kabwe
Zitto Kabwe

Na Zitto Kabwe,

SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria kutunga Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.

Muswada wa Sheria hiyo sasa upo mbele ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuchambuliwa na kisha kuwasilishwa Bungeni.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kanuni ya 84 ya Kamati ya Bunge inawajibika kuutangaza muswada na kupokea maoni ya wadau mbalimbali.

Ni wazi kuwa wadau wa muswada huu ni wananchi wote kwani haki ya kupata habari ni haki ya kikatiba.

Hata hivyo, waandishi wa habari na wamiliki wa vyombo vya habari na mitambo ya kuchapisha magazeti na majarida ni makundi yatakayoathirika moja kwa moja na muswada huu utakapokuwa sheria.

Lakini pia, muswada unapelekwa mbio na Mwenyekiti wa Kamati kutishia kuwa iwapo wadau hawatatoa maoni, kamati yake itaendelea na kazi zake za kutunga sheria.

Kwa muda mrefu sana waandishi wa habari na wanazuoni mbalimbali wamekuwa wakitaka kuwepo na sheria ya kusimamia tasnia ya habari.

Ninaambiwa kuwa juhudi za kutunga sheria hii ni mchakato wa zaidi ya miaka 20, tangu mwaka 1993 ambapo muswada wa kusajili waandishi wa habari uliondolewa bungeni, baada ya kuwasilishwa na Dk. William Shija wakati ule akiwa Waziri wa Wizara ya Habari na Utangazaji, kwa sasa ni marehemu.

Vile vile, kumekuwa na kilio kikubwa cha vyombo vya habari kufungiwa kwa kutumia Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ambayo inampa mamlaka makubwa sana Waziri wa Habari.

Wananchi wengi na wapenda demokrasia walitarajia kwamba sheria mpya ingeweza kuondoa sheria kandamizi na kuweka uhuru wa vyombo vya habari ipasavyo.

Muswada uliopo mbele ya kamati ya Bunge unatoa tafsiri pana sana ya vyombo vya habari. Sehemu ya 3 ya muswada inatamka chombo cha habari ni pamoja na gazeti, kituo cha radio na televisheni ikiwamo mitandao ya kijamii (online platforms).

Muswada unatamka kuwa ni lazima vyombo vya habari viwe na leseni maalumu kwa ajili ya kufanya kazi na waandishi wa chombo hicho ni lazima waandikishwe kwenye chombo kiitwacho Accreditation Board (Bodi ya Ithibati).

Iwapo sheria hii itatungwa maana yake ni kwamba mtandao kama wa jamiiforums, utapaswa kuandikishwa na watu wote wanaotoa maoni yao kwenye mtandao huo lazima wawe na ithibati!

Haitaishia hapo, bali hata blogu zitapaswa kuandikishwa kama ilivyo magazeti. Hatua hii itauminya sana uhuru wa watu kupata habari na kupashana habari. Hata uhuru wa kujieleza utaminywa kupitia mitandao ya kijamii.

Muswada unataka kuwepo na sheria ya Serikali kuamua vyombo vya habari viandike nini na vitangaze nini.

Sehemu ya 7(1) (b) (iv) inatamka wazi kwamba Waziri anaweza kuagiza chombo chochote cha habari cha binafsi kutangaza habari fulani au masuala fulani yenye umuhimu kwa taifa.

Itakumbukwa kwamba muswada uliopita ambao ulikataliwa, ulitaka ifikapo saa mbili usiku televisheni na radio zote ziungane na Televisheni ya Taifa (TBC) kutangaza taarifa ya habari.

Kifungu hiki ndicho kitakachotumika kufanya suala hilo kwa amri ya waziri. Kifungu hiki pia kinampa Waziri wa Habari mamlaka ya kuelekeza chombo cha habari kutotoa habari fulani kwa utashi wa Waziri.

Ni dhahiri kuwa huu ni ukiukwaji mkubwa sana wa uhuru wa habari na kuwa kikwazo kikubwa kwa kazi za waandishi.

Kwa kutumia kifungu hiki, Waziri wa Habari anaweza kuagiza magazeti yote yasiandike habari za IPTL Tegeta Escrow na Waziri atakuwa ndani ya sheria.

Muswada pia unampa Waziri wa Habari mamlaka ya kutoa masharti ya kazi za vyombo vya habari. Hii inatia nguvu kifungu hicho hapo juu kuhusu maelekezo ya habari za kutolewa na kutotolewa na vyombo vya habari.

Muswada huu umerudisha vifungu vyote kandamizi vilivyopo kwenye sheria ya magazeti ya mwaka 1976. Kwa mfano kifungu cha 54-56 kinampa waziri haki ya kutamka kwamba gazeti fulani au kitabu fulani kisisambazwe nchini au kuzalishwa nchini.

Kwenye masuala mengine, Mkurugenzi wa Habari Maelezo na Jeshi la Polisi linaweza kuingia kwa nguvu na kuchukua mitambo inayozalisha magazeti kwa sababu tu gazeti hilo limechapisha habari ambayo kwa maoni ya Serikali, ni habari za kichochezi.

Kwa ufupi, huu ni muswada mbaya kuliko sheria ya magazeti ya sasa. Huu muswada unairudisha nchi nyuma katika juhudi za kujenga taifa lenye haki na wajibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles