Na AMINA OMARI, LUSHOTO
JESHI la Polisi mkoani Tanga kwa kushirikiana na kitengo cha operesheni na mafunzo kutoka makao makuu ya jeshi hilo Dar es Salaam, limewaua watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walipojibizana kwa risasi.
Wakati wa tukio hilo Oktoba 18 mwaka huu wilayani hapa, polisi wawili walijeruhiwa kwa risasi katika misitu ya Kitongoji cha Kitui, Kata ya Kwemshashi wilayani Lushoto.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani, alisema jana kuwa wakati wa operesheni hiyo zilikamatwa bunduki tisa zikiwamo SMG saba, shotgun moja na rifle moja iliyoporwa na majambazi hivi karibuni katika Chuo cha Sekomu.
“Tulikamata pia risasi 425 za SMG na nyingine saba za shortgun, radio saba za mawasiliano ya upepo, bendera nne zenye maandishi ya kiarabu na mavazi manne ya kuficha sura,” alisema Marijani.
Aliwataja majambazi waliouawa kuwa ni Murdick Abdi, maarufu kwa jina la Osama ambaye ni mfanyabiashara pamoja na Sultan Abdallah, mkazi wa Kiembesamaki kisiwani Zanzibar.
“Kabla majambazi hao hawajauawa, walikamatwa na kuwapeleka polisi mahali walipoficha silaha.
“Wakati wako njiani kuelekea eneo hilo, ghafla jambazi mmoja alitamka maneno ya kiarabu kama ishara ya kuwashtua wenzake ambao walikurupuka kutoka mafichoni na kuwashambulia polisi.
“Polisi nao walijibu mapigo na kuwaua majambazi wawili ingawa pia polisi wawili walijeruhiwa kwa risasi,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, alisema operesheni hiyo ni mwendelezo wa hatua za kukabiliana na wahalifu.
Kamanda Wakulyamba aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kukabiliana na wahalifu popote walipo mkoani hapa.
Wakati majambazi hao wakiuawa mkoani Tanga, juzi Dar es Salaam, polisi waliwaua majambazi sita katika eneo la Mbezi kwa Yusuf, Makondeni, wilayani Kinondoni.
Majambazi hao waliuawa walipokuwa wakijibizana kwa risasi na askari wa kikosi maalum cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha.
Pia, Oktoba 17 mwaka huu, majambazi wawili waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki namba MC 370BEY wakiwa na shortgun walivamia duka eneo la Tegeta na kupora fedha na vocha za mitandao ya simu.
Wakati hayo yakiendelea, hivi karibuni majambazi yaliwaua polisi kadhaa eneo la Mbande wilayani Temeke na kupora bunduki.